Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Moshi
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi,amesema serikali inaendelea kuboresha maisha ya wananchi.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira hususan matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki wa mazingira.
Dkt.Nchimbi amesema hayo Juni 5, 2024 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Tusitegeane tukifikiri wengine wana wajibu mkubwa kuliko wengine,”amesema.
Kuhusu utunzaji wa mazingira, alitoa wito kwa wananchi hao kuacha utamaduni wa matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamechangia uharibifu wa mazingira na afya za watumaji.
Amesema kwa sasa matukio ya mto katika mlima Kilimanjaro yamepungua kwa sababu ya juhudi za uhifadhi mazingira, suala ambalo linapaswa kuendelezwa.
Katika hatua nyingine Dkt.Nchimbi amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka majaribio ya watu kufikiri kila mtu anaweza kuwa kiongozi au kila chama cha siasa kinauwezo wa kuongoza nchini.
Pia amesema lazima ifahamike kwamba hakuna chama cha siasa chenye uwezo wa kupewa dhamana ya kuongozaa nchi na watu wakalala usingizi zaidi ya CCM.
“Mnasikia vyama vya upinzani viongozi wake wakitupiana maneno,Wakati mwingine tuwape muda, tuliwapa miaka 20 tukaona bado, tuwape miaka 20 mingine tuwaangalie huwenda wakakomaa,”amesema Dkt.Nchimbi.
Vilevile amezungumzia suala la utalii ambapo amesema utalii nchini umefunguka zaidi kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt. Samia ya kutangaza vivutio kupitia filamu ya Royal Tour.
“Ni Rais wa kwanza kufanya filamu ya kutangaza utalii hivyo tunawajibu wa kunufaika na matunda ya biashara hiyo kupitia kuimarisha biashara na tutakuwa na mashindano ya AFCON, lazima tujiandae na moja ya mkoa ni Kilimanjaro,”amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla,ameeleza kuwa wanachama wengi kutoka vyama vya upinzani wamempigia simu kwamba wanataka kuhamia CCM.
Amesema amekuwa akipokea simu nyingi za wanachama hao kutaka kujiunga CCM kwa sababu ya vyama vyao kuwepo migogoro.
“Huko upande wa pili hali ni tete, kuna migogoro kibao na kila siku napokea simu watu wanauliza wanataka kurejea CCM hata leo asubuhi nimepokea simu watu wanaomba kurejea CCM,”ameeleza.
Naye Mbunge wa Moshi Mjini (CCM) Priscus Tarimo,amesema Rais Dkt. Samia ameleta neema katika sekta ya utalii kwani ada ya waendesha shughuli za utalii imeshuka kutoka dola 2000 hadi dola 1000 kwa mwaka.
Pia,amesema ada kwa wasindikizaji watalii ambayo ilikuwa dola 50 kila mwaka, sasa imeshuka hadi sh. 100,000 kila baada ya miaka mitatu.
Ameeleza kuwa katika vipaumbele 10 vya jimbo hilo, tisa vimepatiwa fedha na vipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji na kimoja ambacho Moshi kuwa jiji suala hilo lipo katika hatua ya maamuzi.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato