December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nchimbi:Fedha isitumike kama kigezo kuchagua kiongozi

Na Agnes Alcardo,Timesmajiraonline, Singida

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi, ametoa onyo kwa viongozi wa Chama hicho nchini ngazi zote, kutotumia kigezo cha mtu mwenye fedha nyingi kuwa ndiye anayefaa kuwa kiongozi wa Chama na kusema sifa ya kiongozi ni yule mwenye uwezo na utayari wa kuhudumia wananchi.

Dkt.Nchimbi alitoa maagizo hayo Jijini Singida katika mkutano wa ndani uliohusisha viongozi na wanachama wa CCM, mabalozi watendaji wa serikali pamoja na wananchi.

Amesema wakati huu ambao CCM inajiandaa kuingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, Chama kinapaswa kusimamisha wagombea wenye kukubalika kwa uwezo wao wa kutatua changamoto za wananchi, heshima kwa jamii na ushirikishaji.

“Viongozi kataeni kutumika, msichague viongozi kwa sababu ya fedha bali tengenezeni ramani ya kuwapata viongozi bora, mkatae kuyumbishwa, wapimeni watu kwa uwezo wa kuongoza, kuheshimu na pale shida za wananchi zinavyowagusa kwani sifa Kuu ya kiongozi ni kufahamu nafasi wanazotumikia ni kwa ajili ya wananchi.

Wengine wanatafuta nafasi kwa fursa, viongozi washawishini watu kugombea kwa kutambua wanamoyo wa kuwatumikia wenzao.” amesema Nchimbi.

Pia amesema kuwa, uongozi wa chama cha siasa ni kushirikisha siyo kuongoza kama kampuni.

“Viongozi hatupo badala ya wanachama, tupo kwa niaba ya wanachama. Ukiwa mwenyekiti shirikisha kamati ya siasa ukiwa katibu shirikisha sekretarieti. Huo ndiyo uongozi,”amesisitiza Dkt.Nchimbi.

Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla,amesema utekelezaji ilani ya uchaguzi ya CCM umefanyika kwa mafanikio mengi.

Amesema mafanikio hayo sifa zote ni kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ameleta fedha nyingi za maendeleo kuliko awamu zote na kila mmoja anakubaliana na hilo hususani wabunge.

“Mafanikio haya tuyaseme wakati wote hata balozi anapaswa kuyasema, kuna wale wanaosema sasa hivi watanzania wamekuwa machawa yani kila kitu wanamtaja Samia..sasa wanataka tumtaje nani? Hata wao familia zao zinawapongeza na kuwashukuru pale zinapiwafanyia mambo mazuri ndiyo maana na sisi tunamshukuru Rais pale anapotufanyia mazuri na ndiyo utamaduni wetu kushukuru,”amesema Makalla.

Ameongeza kuwa, “Hatuwezi kurudishwa nyuma kwani maendeleo tumeyaona, tutaendelea kumshukuru Rais Samia. Jambo hili zuri la kumpongeza Rais Samia, tutaendelea nalo,”amesisitiza.

Hata hivyo,ametoa msisitizo wa kusikiliza kero za wananchi kisha kuzitatua huku akiagiza viongozi wa Chama nao kusikiliza kero,”Tusiwe mabingwa wa kusikiliza kero, tuwape majawabu. Msisitizo wangu tusiwaachie watendaji wa serikali pekee tufungue ofisi za chama kusikiliza kero za wananchi,”amesema.