Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt.Emmanuel Nchimbi amepokelewa na mamia ya wanachama wa Chama hicho katika ofisi za Makao Makuu mkoani Dodoma huku akiwataka wanachama wa chama hicho kukitetea chama hicho kwa kuyazungumza yale yote yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha wanachama watatu chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho wamehamia CCM .
Akizungumza katika hafla fupi ya mapokezi yake ,Dkt.Nchimbi amewataka wanaCCM kujenga tabia ya kukitetea CCM katika majukwaa mbalimbali ikiwemo katika mitandao ya kijamii kwani Rais Samia Suluhu Hassan ni mtaji tosha wa chama hicho kutokana na mambo mengi aliyoyafanya katika kipindi kifupi cha utawala wake.
“Ni muhimu kwa wanachama wote kukitetea chama chetu katika maeneo yote hadi kwenye mitandao ya kijamii,na tukitete kwa hoja siyo kwa lugha za matusi wala kejeli,
“Na Rais wetu tayari ni mtaji wa chama,amefanya mambo mengi mazuri,tumzungumzie wala tusione haya ,kazi zake zinamtambulisha.”amesema Dt.Nchimbi
Kwa upande wake Peneza amebainisha kilichomsibu mpaka kukihama Chadema ni utendaji mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba ni Rais mwenye kuleta mabadiliko nchini.
“Nimekuwa CHADEMA kwa miaka 15 ,hivyo nimekuwa na tafakari ya muda mrefu katika safari hii ya kuhamia CCM ,nikafanya mawasiliano na viongozi wakakubali kunipokea ,
“Kwa hiyo niseme tu kwamba nilikuwa CHADEMA kwa sababu nilikuwa na kiu ya kuleta mabadiliko nchini kwetu ,lakini sioni haja ya kuendelea kubaki huko kwa sababu Rais Samia anafanya mabadiliko ya nchi kwa vitendo.
“amesema Peneza
Alisema Rais Samia ni msikivu ambapo licha ya kutukanwa na kukebehiwa lakini kwa usikivu wake amekuwa akichukua yale ya muhimu na kuyafanyia kazi .
Kuhusu maandamano amesema upinzani hawakuwa na sababu ya kupanga wala kuandamana wakati huu kwa sababu Serikali imepokea maoni tu ya Muswada wa sheria ya Uchaguzi ambayo ndio inaenda kujadilwa Buungeni.
“Kama wanataka kuandamana ,wangesubiri miswada hiyo ijadiliwe bungeni na kuona nini kimechukuliwa na nini kimeachwa kwa sababu Serikali haijasema kwamba imekataa maoni kuhusu miswada hiyo”alisisitiza
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi