Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) ameipongeza Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kuanzisha moduli ya kuwasilisha rufaa/malalamiko kwa njia ya kieletroniki.
Dkt. Mwigulu ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la PPAA katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), na kusema kuwa anaamini moduli hiyo itaisaidia kupata thamani halisi ya fedha.
“Napenda kuwapongeza PPAA kwa kuanzisha Moduli hii, nawasihi muendelee kufanya kazi kwa bidii na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu amefunga rasmi Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki lililoanza tarehe 9 – 12 Septemba, 2024 Jijini Arusha.
Awali Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, PPAA imeweza kushughulikia jumla ya mashauri 140 yaliyotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma.
“Mhe. Waziri katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 32 zenye thamani ya Bilioni 567/- kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika,” amesema Bw. Sando na kuongeza kuwa hatua hiyo imesaidia kuepusha utekelezaji usioridhisha wa miradi unaosababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best