November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango:Wizara ya afya endeleeni kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji Magonjwa

Na.Mwandishi wetu,timesmajira, Online

Makamu wa Rais wa Tanzania,Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Afya kuendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa mwenendo wa magonjwa ya kuambukiza hususani magonjwa hatarishi.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo leo tarehe 16/7/2022 wakati akifungua Maabara ya Afya ya Jamii ngazi ya 3 ya usalama iliyoko kwenye hospitali Maalumu ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro.

Amesema Wizara inatakiwa kuhakikisha tetesi yoyote ya ugonjwa inayotokea nchini inafanyiwa uchunguzi kwa wakati ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa wananchi kama tatizo hilo halikujulikana kwa wakati.

Aidha, Dkt. Mpango ameitaka Wizara ya Afya kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kutumia vituo vya afya na zahanati za Serikali na hata za binafsi ambazo zipo karibu na wananchi kwa ajili ya kutoa huduma za kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza.

“Nimepewa taarifa kuwa ni asilimia 20 tu ya vituo binafsi vya afya ndivyo vinatoa huduma za Kifua Kikuu, ni vyema kujua changamoto na kuweza kutatuliwa”.

Hata hivyo amewataka Viongozi wote ngazi ya kijiji, kata na Wilaya kuendela kuimarisha kamati za afya za kijiji ili kuimarisha huduma za afya za wananchi wa eneo hilo.

Vile vile Dkt. Mpango amewataka Watanzania kufuata maelekezo ya wataalamu kwani ugonjwa wa Kifua Kikuu unatibika na hivyo mara waonapo dalili waweze kuwahi kituo cha afya.

Makamu huyo wa Rais amewataka wananchi kujijengea tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kama kuna dalili za ugonjwa na ikibainika waweze kutibiwa kwani magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ya kuambukiza yanaweza kutibika na kupona yakiwa katika hatua ya awali.