January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango:Viongozi mtakaochaguliwa, uchaguzi wa serikali za mitaa tumieni nafasi zenu vizuri

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kutumia vema nafasi hizo kuwaletea wananchi maendeleo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo mara baada ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kitongoji cha Kihanga Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Amesema ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa viongozi hao kwa kujitokeza kuwaunga mkono katika shughuli za maendeleo watakazosimamia.

Makamu wa Rais amewapongeza wanakijiji wote waliojitokeza katika uchaguzi huo kwa kuwa ni muhimu kwa msingi wa maendeleo. Amesema viongozi wa serikali za mitaa ni viongozi wa ngazi ya msingi wanaobeba dhamana ya kuwaongoza wananchi kupata maendeleo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kijiji hicho na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani mara baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kushiriki vema kwa utulivu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Pia amewahimiza kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuhakikisha watoto wa eneo hilo wanapata elimu mashuleni kikamilifu ili wawe na mchango katika ujenzi wa Taifa.