December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango:Matukio ya ajali barabarani yasipochukuliwa hatua madhubuti,yatakuwa chanzo kikubwa cha vifo ifikapo 2030



Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Taifa linapoteza nguvukazi kubwa sana kutokana na ajali za barabarani ambapo kwa takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani mwaka 2023 zinaonesha kuwepo kwa matukio ya ajali za barabarani 1,733 ambapo vifo vilivyotokana na ajali hizo vilikuwa 1,647 (sawa na ongezeko la 6.6.%, ikilinganishwa na vifo 1,545 mwaka 2022).

Amesema inakadiriwa kwamba endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kukabiliana na hali hiyo, ajali mbaya za barabarani zitakuwa ndiyo chanzo kikubwa cha vifo nchini ifikapo 2030.

Dkt.Mpango amesema hayo jijini hapa leo,Agosti 26,2024,wakati akifungua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri,yanayokwenda na kauli mbiu isemeyo “Endesha Salama, Ufike Salama”

Amefafanua kuwa ajali zinazohusisha pikipiki zimekuwa nyingi na zinaongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kipindi cha Januari hadi Desemba 2023 kulikuwa na jumla ya matukio  435 ya ajali za pikipiki yaliyoripotiwa.

“Katika kipindi hicho hicho, idadi ya vifo vilivyotokana na ajali za barabarani zinazohusisha pikipiki ilikuwa 376 ikilinganishwa na vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022 (sawa na ongezeko la 13.3%),”amesema.

Hivyo amesema katika kudhibiti ajali za pikipiki ni muhimu kuendelea kusimamia sheria hususan katika uvaaji wa kofia ngumu, kutobeba abiria wengi kwenye pikipiki moja na umiliki wa leseni halali ya udereva pamoja na bima ya chombo cha moto huku akiwasihi waendesha pikipiki wote maarufu kama bodaboda wote wajiunge na Shirikisho lao na wakate bima kwa ajili yao wenyewe na vyombo vyao vya moto.

Akizungumzia maadhimisho hayo Makamu wa Rais Dkt.Mpango amesema ili kupata manufaa ya maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, ni lazima kuacha kufanya maadhimisho hayo kimazoea bali yalenge kubadili fikra na mwenendo wa wananchi wanapotumia barabara.

Amesema ukaguzi wa magari unapaswa kuwa endelevu na kufanyika kwa mwaka mzima hasa kwenye mabasi angalau hata mara mbili kwa mwaka badala ya kusubiri hadi kwenye Wiki ya Usalama barabarani Kitaifa.

Aidha amesema kuwa makosa ya kibinadamu ndiyo chanzo kikubwa cha ajali nchini, hakuna budi kuelekeza nguvu katika kudhibiti vihatarishi mahsusi vitano ambayo ni mwendo kasi, kuendesha chombo cha moto katika hali ya ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutofunga mikanda ya usalama katika gari pamoja na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wawapo ndani ya magari.

Aidha ametoa rai kwa wananchi na hasa abiria katika vyombo vya usafiri kukemea au kutoa taarifa za uvunjifu wowote wa Sheria za Usalama Barabarani, hususan kuhusu uendeshaji wa mwendokasi na usio salama au uharibifu wa barabara na miundombinu yake.

Pamoja na hayo amesisitiza umuhimu wa udhibiti wa magari yanayobeba wanafunzi kwa kuwa magari mengi yana hali mbaya inayotishia usalama wa wanafunzi na madereva wenyewe.

Amesema baadhi ya madereva wa magari hayo wameonekana kukosa weledi na uadilifu hali inayosababisha madhara mbalimbali zikiwemo ajali mbaya.

Hata hivyo Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuwekeza katika TEHAMA ili kudhibiti kirahisi ajali na makosa mengine ya usalama barabarani,pia amesisitiza kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia njia mbalimbali hususan vyombo vya habari, machapisho mbalimbali, maonesho, sanaa na muziki, mikutano ya hadhara pamoja na njia ya mitandao ya kijamii ili kuyafikia makundi yote ya watumiaji wa barabara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo amesema Baraza hilo limeandaa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ajali ambao ni shirikishi. Amesema Mkakati huo umelenga mambo mbalimbali ikiwemo udhibiti wa madereva walevi na wazembe, udhibiti wa mwendokasi kwa madereva, kuwashirikisha wamiliki wa vyombo vya moto katika dhana ya uwajibikaji.

Ameeleza kuwa mkakati huo unalenga kudhibiti uendeshaji wa magari bila sifa na kutokuwa na bima, udhibiti wa usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo, kudhibiti ajali za pikipiki na bajaji, kuhakikisha abiria wanafunga mikanda wanapotumia vyombo vya usafiri, kutambua na kudhibiti maeneo hatarishi yanayosababisha ajali.

Pia Kuanza kutumika kwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za madereva ili kuondoa wale wanaokithiri kwa kukiuka sheria pamoja na kurekebishwa kwa sheria za barabarani ili kuendana wakati pamoja na matumizi ya Tehama katika kusimamia sheria.

Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi limebuni mifumo mbalimbali ya kielektroniki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa serikali ili kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa magari ya abiria ambapo ametaja mifumo hiyo ikiwemo mfumo wa utoaji leseni, mfumo wa kutoa taarifa za ajali pamoja mfumo wa malipo ya faini.

Amesema kwa mara ya kwanza mwaka 2024 Kikosi cha Usalama Barabarani kimeweza kutoa huduma ya ukaguzi wa vyombo vya moto na utoaji wa stika za usalama barabarani kupitia mfumo wa malipo wa serikali (GePG).

“Mfumo wa Kielektroniki wa usajili wa madereva wanafunzi utazinduliwa hivi karibuni utakaowezesha Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani kuweza kufuatilia kila mwanafunzi aliyesajiliwa ili kutambua kama anastahili kupata leseni ya udereva.