Na Mwandishi wetu , timesmajira
MAKAMU wa Rais Dkt, Philip Mpango anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Jukwaa la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali linalotarajia kufanyika Oktoba 3 hadi 5, mwaka huu katika ukumbi wa Mkutano wa Jakaya Kikwete Dodoma ambapo mashirika takribani 9,000 yaliyopo chini ya mwamvuli wa baraza hilo yanatarajia kuwakilishwa katika mkutano huo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Afisa Mtendaji Mkuu NaCoNGO, Racheal Chagonja amesema mkutano huo huwa unafanyika kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu jukwaa hilo, linatarajia kuanza Oktoba 3 hadi 5 huku washiriki zaidi ya 2,000 ambao ni wawakilishi wa mashirika hayo wanatarajia kushiriki mkutano huo.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuibua mijadala mbalimbali ikiwemo suala la fursa pamoja na kutatua changamoto zinazoendelea kuikumba sekta ya mashirika hayo ambayo sio ya kiserikali na kutafuta majawabu ya changamoto zao katika kurahisisha utendaji kazi.
”Mkutano huu unafanyika kila mwaka na huwa unatanguliwa na mikutano ya ngazi za mikoa ambapo mikutano hiyo inaibua mambo mbalimbali yanaletwa katika Jukwaa la Taifa na kujadiliwa kwa upana wake,” amesema na kuongeza
”Kupitia mkutano huu unaleta mabadiliko makubwa kwa yale yanayotakiwa kubadilika mfano katika masuala ya kisera, kiutendaji, maadili na namna ya mashirika kujisimamia yenyewe bila kutegemea fedha za wafadhili,” amesema.
Amesema katika mkutano huo utakaochukua takribani siku tatu, utakuwa na programu mbalimbali ikiwemo ya uwajibikaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa jamii ambapo watakuwa na zoezi la uchangiaji wa damu, upandaji miti pamoja na kwenda kutembelea Kituo cha watoto yatima cha Miyuni mkoani humo.
”Dhamira yetu kubwa katika uchangiaji damu ni kuangalia na kulinda afya ya mama na mtoto, tunaamini kuwa damu tutakayochangia itaweza kuchangiza watu kusaidia makundi hayo, mbali na hilo tutakuwa na zoezi la utoaji wa huduma za kisheria ambapo kama mwananchi yoyote mwenye shida ya kupata msaada wa kisheria tunamkaribisha kufika katika viwanja vya ukumbi huu na kuweza kusaidiwa,” amesema .
Amesema pia kupitia mkutano huo wataweza kuendesha mada mbalimbali Oktoba 4, 2023 ikiwemo kuangalia fursa za ndani na nje ya nchi za ufadhili wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo watapata fursa ya kuangalia ni namna gani miaka michache ya nyuma imekuwa na upungufu wa fedha za wafadhili kwaajili ya kusaidia mashirika kufanya kazi zake .
”Hii imefanya mashirika mengi kukwama kutokana na kutegemea fedha hizi za wafadhili, tunaamini kwa kupitia mjadala huo tutaweza kuleta mawazo mapya namna gani tutaweza kutumia rasilimali za ndani kuhakikisha mashirika yanaendelea kupata ushirikiano katika kufanya kazi zake,”amesema na kuongeza
”Mada nyingine itaweza kuongelea Mifumo ya kisera na kisheria ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ambapo tutaangalia fursa na changamoto za mifumo ya sheria ambazo zimekuwa vikwazo katika uratibu na utendaji wa mashirika hayo tangu sheria ya mashirika imeanzishwa miaka 23,” amesema.
Amesema eneo lingine wataweza kuangalia namna gani mashirika hayo yasiyo ya kiserikali kuwa na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo yatapaswa kujiangalia wenyewe mashirika namna watakavyokabiliana na mabadiliko hayo kabla hawajapeleka miradi kwa wananchi.
”Ni lazima mashirika yawajibike kuchagiza maendeleo ya nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwani mara nyingi tunapokea fedha za miradi hatujiangalii ndani wenyewe kwenye taasisi zetu namna tunavyoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kisha kuyapeleka nje,”amesema.
Aidha alisema wataweza kuangalia namna gani teknolojia na ubunifu utakavyoweza kusaidia na ustawi wa mashirika.”Kwani siku hizi teknolojia imekuwa kipaumbele sana na kila kitu kimekuwa kidigitali hivyo tutaangalia teknolojia na ubunifu unaendana vipi na ukuaji wa sekta yao katika kuhakikisha wanafanya tafiti pamoja na data ambazo zinatija ili watu waelewe,”amesema.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa