Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Dkt,Philip Mpango amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaotoa lugha za hovyo dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifanya kazi ya kuhakikisha Taifa linafikia mipango ya maendeleo iliyojiwekea.
Dkt,Mpango amesema hayo Mkoani Mbeya alipokuwa akifungua maonyesho ya sherehe za wakulima Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya .
“Kuna watu ambao wamepewa fursa na Mh. Rais lakini wamekuwa wakitoa lugha za hovyo za kumkashifu na nawasihi kuacha tena nasisitiza waache”amesema Dkt.Mpango nakuongeza kuwa
“Wapo watu wanaosema Makamu wa Rais yuko kimya, siyo kwamba sisikii, haya mambo yanahitaji busara sana.”
Katika hatua nyingine ,Dkt. Mpango ,amewaagiza wakuu wa Mikoa Nyanda za Juu Kusini , kufuatilia masuala ya matumizi mabaya ya viuwatilifu,uingizwaji holela wa mifugo jambo ambalo libasababisha migogoro ya wakulima na wafugaji .
“Kuna changamoto katika Kanda hii mifugo inaingizwa kiholela na kusababisha watu kuuwawa,mifugo kama tembo kuingia kwenye makazi ya watu na kufanya uharibifu”alisema.
Aidha amewataka wakuu wa Mikoa kudhibiti mifugo ikiwepo kutenga maeneo ya kilimo na ufugaji hususan ujenzi wa majosho na kuuzwa kwa mifugo ya ziada .
Katika hatua nyingine ,ameitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha maeneo yote ya vituo vya utafiti nchini kulindwa ikiwa ni pamoja na maeneo hayo kupewa hati miliki ili kudhibiti kuvamiwa na wananchi.
“Kumeibuka mtindo wa watu kuvamia maeneo ya vituo vya utafiti na kuendekeza makazi watendaji wa maeneo husika mkasimamie hilo kwa ili kulinda usalama wa chakula unaotokana na tafiti zinazofanywa”amesema.
Kwa upande wake ,Waziri wa Kilimo ,Hussein Bashe ameonya viongozi wa kisiasa Mkoa wa Mbeya kutokuwa chanzo cha kuwatetea wananchi wa eneo la Sae waliovamia eneo la utafiti wa kilimo Tari -Uyole.
“Nilifika hapa jioni nikiambatana na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini ,Dkt. Tulia Ackson nilitoa maelekezo na kusitisha ujenzi lakini mnakiuka maagizo ya Serikali na kuwasikiliza wanasiasa ambao wanawadanganya ”amesema Bashe na kuongeza kuwa
“Nikiwa kama Waziri mwenye dhamana ,sintasita kuvunja nyumba zinazoendelezwa katika eneo hilo kwa sababu eneo lilishatengwa kwa ajili ya matumizi ya utafiti ambao matokeo yake ni kwa ajili ya kulinda usalama wetu sote”.
Naye Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini ,Dkt. Tulia Ackson ,kwa niaba ya wabunge wa Jimbo la Mbeya wameishukuru Serikali kwa kuwekeza kwenye elimu ikiwepo ujenzi wa shule mpya za Dkt.Tulia Ackson,Iziwa na Mwakibete.
Aidha ameiomba Serikali kuongeza idadi ya vijana kwenye mradi wa kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko ( Building a Better Tomorrow-BBT) ili kuboresha sekta ya kilimo na kuweza kujiajiri.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato