December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mollel:Hakuna Wilaya itakayokosa magari ya wagonjwa

Na Rayson Mwaisemba, WAF- LINDI.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imenunua jumla ya magari mapya ya kubebea wagonjwa 720 yatayofanya kila Wilaya kuwa na gari la kubebea wagonjwa hivyo kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ilulu Mkoani Lindi yenye kauli mbiu ya “Imarisha usawa.”

Sambamba na hilo amesema Dkt. Mollel amesema, katika kipindi kifupi tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani zaidi ya CT-SCAN 34 zimenunuliwa zitazofungwa katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na kuwasaidia wananchi kupata huduma hizo ambazo ilikuwa historia kuzipata hapa nchini.

Ameendelea kusema kuwa, CT-SCAN moja ni zaidi ya Bilioni 2.2 hivyo kutoka hospitali mbili za Rufaa za Mikoa zilizokuwa na CT-SCAN mpaka kufikia hospitali zote za Rufaa za Mikoa kuwa na mashine hizo ni msaasa mkubwa sana katika kuwapunguzia wananchi gharama za matibabu na usumbufu wa kutafuta huduma hizo uliokuwa hapo awali.

Amesema kuwa zaidi ya miliini 180 zilikuwa zikitumika katika gharama zote za kusafirisha mgonjwa kufuata huduma za CT-SCAN hivyo upatikanaji wa mashine za CT-SCAN umesaidia kuokoa gharama kubwa ambazo zingetumika kwenye kusafirishia wagonjwa, na sasa gharama hizo zinatumika katika kuboresha huduma nchini.

Pia, Dkt. Mollel amesema, Serikali imenunua mashine ya Pet Scan itayosaidia kutibu sehemu yenye tatizo la Ugonjwa wa kansa bila kuathiri eneo lingine lolote ikiwamo kunyonyoka nywele, huku akisisitiza kwa Afrika Mashariki na kati Tanzania ni nchi pekee yenye mashine hiyo itayosaidia kuzalisha mionzi dawa.

Kwa kununua mashine hiyo kumsaidia kupunguza gharama za matibabu na kuokoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 5 iliyokuwa ikitumika kununua mionzi dawa katika nchi ya Afrika Kusini ili kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa huduma hizo. Amesisitiza Dkt. Godwin Mollel.

Mbali na hayo Dkt. Mollel amesema, Serikali imenunua mashine ya angio suite kwaaji ya matibabu ya watoto wenye tatizo la ulimi mkubwa, na tayari zaidi ya watoto 500 wamepatiwa huduma hiyo katika taasisi ya MOI, huku kila upasuaji wa mtoto mmoja ungegharimu kiasi cha shilingi milioni 100.