November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mabula ataka wananchi kuchangamkia zoezi la urasimishaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Amgeline Mabula amewataka wananchi kuchangamkia zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini ili kuondokana makazi holela.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo tarehe 1 Machi 2023 mkoani Arusha wakati wa zoezi la kukabidhi Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata za Muriet na Olasiti mkoani humo.

Zoezi la urasimishaji makazi holela ni zoezi la miaka kumi na lilianza mwaka 2013  na linatarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2023.

“Serikali inaendelea na program ya kupanga na kupima ardhi ikiwa na lengo la kuondoa makazi holela, program hii inafanyika katika meneo mbalimbali ilianza mwaka 2013 na inategemea kuisha mwaka huu” alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mkoa wa Arusha una jumla ya mitaa 112 inayofanyiwa urasimishaji ambapo michoro ya mipango miji 391 imeandaliwa na kuidhinishwa yenye viwanja 104,097 na tayari viwanja 55,023 vimewekewa beacon huku upimaji wa viwanja 46,197 ukiwa umeidhinishwa.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesikitishwa na muitikio mdogo wa wananchi waliojitoleza kuchangamkia zoezi hilo la urasimishaji makazi holela nchini.

Amesema, takwimu katika zoezi hilo kwa kata ya Olasiti inaonesha kuwa hadi sasa ankara 4,009 zimetolewa kwa wananchi lakini ni wananchi 934 tu ndiyo waliowasilisha maombi ya hati na kati ya hao ni 517 waliochukua hati zao.

Aliwasihi wananchi waliorasimishiwa makazi yao kuhakikisha wanalipa kwa wakati gharama za kurasimishiwa maeneo yao ili zoezi la urasimishaji katika mitaa yao  liishe kwa wakati.

Amesema, wizara ya ardhi kwa kuhirikiana na wadau wote wanaoguswa na shughuli za urasimishaji itaendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kutatua kero za wananchi zilizobainika katika halmashauri zinazotekeleza kazi za urasikishaji.

Aliwakumbusha wananchi kuhusu msamaha wa riba ya kodi ya ardhi uliotolewa na mhe rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutaka wadaiwa wakubwa kutumia fursa hiyo kabla haijaizha tarehe 30 April 2023 kwa kuwa kumekuwa na kawaida kwa wananchi kulalamika kwamba wanaomba kuongezewa muda ikifika mwisho wa siku za msamaha.

Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Gasper alisema, pamoja na serikali kuamua kuwarasimishia makazi wananchi lakini tatizo linaonekana lipo kwa wananchi kutokana na kwa kushindwa kulipia gaharama za kurasimishiwa na wengine kushindwa kuchukua hati ambapo aliwaomba wananchi wa mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa ya zoezi la urasimishaji kabla halijafungwa.

“Sitegemei kuona wananchi wanakuja ofisini kuomba kuongezewa muda na kuwataka kuutumia muda wa sasa vizuri kwa kurasimishiwa makazi yao kutaka uhamasishaji zaidi kwa wananchi katika zoezi hilo” alisema Gasper

Kamishna wa ardhi Msaidizi mkoa wa Arusha Idrisa Kayera aliweka wazi kuwa, kwa sasa muitikio wa kuchukua hati kutoka kwa wananchi waliorasimishiwa maeneo yao ni mdogo na kutoa rai kwa wananchi kulipia ankara kwa wakati ili waweze kupatiwa hati.

Diwani wa kata ya Ilerai Losoiki Laizer ametaka wananchi kuhakikisha wanalipia gharama za urasimishaji ili waweze kupatiwa hati kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi na kutaka uhamasishaji zaidi kutoka kwa viongozi mbalimbali.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi  Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata za Muriet na Olasiti mkoani Arusha tarehe 1 Machi 2023.
 
Sehemu ya wananchi wa kata za Muriet na Olasiti mkoani Arusha wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kukabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi tarehe 1 Machi 2023.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Gasper akizungumza katika zoezi la kukabidhi  Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata za Muriet na Olasiti mkoani Arusha tarehe 1 Machi 2023.
Diwani wa kata ya Ilerai mkoani Arusha Bw. Losoiki Laizer akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi hatimiliki kwa wananchi waliorasimishiwa makazi holela tarehe 1 Machi 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikabidhi hatimiliki za ardhi kwa mume na mke wakati wa zoezi la kukabidhi  Hatimiliki za Ardhi kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao kwenye kata za Muriet na Olasiti mkoani Arusha tarehe 1 Machi 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
 
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Arusha Idrisa Kayera akizungumza katika zoezi la kukabidhi hatimiliki kwa wananchi waliorasimishiwa makazi holela tarehe 1 Machi 2023.



Â