Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa wito kwa Benki na Taasisi za Fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kutafuta mbinu za kuwezesha mikopo ya nyumba iwe na riba nafuu ili kuwawezesha wananchi hususan wenye kipato cha chini waweze kumudu mikopo hiyo.
Dkt Mabula ametoa wito huo tarehe 17 Februari 2023 jioni wakati wa hafla ya utiaji saini Makubaliano na uzinduzi wa mikopo wa nyumba ya Benki ya ABSA Tanzania na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Kupitia makubaliano hayo na NHC, Benki ya ABSA Tanzania itakuwa ikifadhili ununuzi wa nyumba za makazi kabla ya kukamilika.
‘’Sote tunafahamu uwekezaji katika sekta ya nyumba unahitaji kiasi kikubwa cha fedha hivyo Benki na Taasisi za fedha zina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya nyunba nchini’’ alisema Dkt Mabula.
Alisema, zipo jitihada zinazofanywa na serikali zinazoigusa sekta ya fedha ikiwemo kuanzisha mradi wa mikopo ya nyumba uliopelekea kuanzishwa Taasisi ya Tanzania Mortage Refinance Company (TMRC) mwaka 2010 na kuanzisha mfuko wa mikopo midogo midogo ya nyumba mwaka 2015.
Takwimu zinaonesha kuwa toka kuanzishwa Taasisi ya TMRC jumla ya Benki na Taasisi za fedha 32 zinatoa mikopo ya nyumba ikilinganishwa na benki 3 zilizokuwa zikitoa huduma hiyo mwaka 2010. Aidha, jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 522.95 imetolewa kwa wateja 5,992 na riba inayotozwa kwenye mikopo ya nyumba imepungua kutoka wastani wa 15%-18% mwaka 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, pamoja na changamoto ya riba ya mikopo ya nyumba bado Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba hususan nyumba bora na za gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imeonesha idadi ya watu nchini ni 61,741,120 ambapo kasi ya kuongezeka ni 3.2% huku idadi ya majengo ikiwa 14,348,372 na mahitaji ya nyumba kwa mwaka yakiwa 390,981.
Kwa takwimu hizo alieleza inaonesha kwa namna gani kasi ya Taasisi za uendelezaji milki kuzalisha nyumba bado ni ndogo na ongezeko la idadi ya watu linachochea pia mahitaji zaidi ya nyumba na kuweka wazi kuwa jitihada zinazofanywa na Benki ya ABSA Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zinaipa faraja serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
‘’Matokeo ya awali ya sensa ya watu na makazi yanaonesha kasi ndogo ya ujenzi wa nyumba na unaochukua muda mrefu. Nitoe rai kwa wadau wote katika sekta ya uendelezaji milki kuona namna ya kutumia teknolojia za kisasa ili kuwa na ujenzi wa nyumba nyingi kwa muda mfupi na gharama nafuu’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemiah Mchechu alisema makubaliano yaliyoingiwa baina ya Shirika lake na Benki ya ABSA Tanzania yatasaidia kutoa changamoto kwa wadau wengine walioingia makubaliano na Shirika hilo.
‘’Tuna partnership na mabenki ishirini lakini nafikiri niseme Benki iliyowasoma na kuwaelewa watanzania vizuri ni ABSA, mmewasoma na mmetuelewa kwa hiyo nawapongezeni sana katika hilo’’ alisema Mchechu.
Kwa mujibu wa Mchechu, NHC imewasoma vizuri watanzania na kuamua kuja na miradi mingi inayolenga soko la kati na chini kati na kutolea mfano miradi ya Samia Housing inayokwenda kutekelezwa nchi nzima na kulenga zaidi mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mkurugenzi wa Benki ya ABSA Tanzania Abdi Mohamed alisema anafahamu changamoto wanazopata watu kuhusiana na ujenzi wa nyumba ambapo alitolea mfano wa uelewa mdogo kwenye suala hilo.
‘’ Watu wengi wanajenga nyumba kwa akiba wanayojiwekea na wengine huwachukua miaka kumi hadi kumi na tano kukamilisha ujenzi, Benki ya ABSA inachofanya ni kujenga uelewa kuwa watu wanaweza kuwa na nyumba kwa muda mfupi na kufanya malipo kidogo kidogo’’. Alisema Mohamed.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato