December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kiruswa atoa maagizo matano kwa tume,wadau wa sekta ya madini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ametoa maelekezo matano kwa Tume na wadau wa Sekta ya Madini nchini,kuhakikisha Watanzania wanajengewa uwezo ili kuendana na soko la ajira katika sekta ya viwanda

Akifunga Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini leo Mei 24, 2024 kwenye Ukumbi wa AICC jijini Arusha, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika sekta hiyo ikiwemo kuendeleza ushirikiano na wadau wa madini ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri hivyo ni muhimu viwanda vinavyojengwa kwenye migodi viende sambamba na kuwapa ujuzi Watanzania.

“Ujenzi wa viwanda kwenye migodi, vinahitaji ujuzi sio kuanzisha tu, nitoe wito uanzishwaji wa viwanda uende sambamba na watanzania kujengewa uwezo,”amesema Dkt. Kiruswa

Dkt.Kiruswa ametoa agizo la pili kwa wawekezaji wa migodi ni kutoa udhamini kwa mafunzo yanayofanyika nje ya nchi kwa watumishi wao ili kuwajengea uwezo.

Pia, Dkt. Kiruswa ameagiza vyuo kufungamanishwa na wawekezaji wa viwanda ikiwemo kuandaa Mitaala ili kuendana na mahitaji ya soko husika.

Dkt. Kiruswa pia ameagiza kuanzishwa kwa program maalum za kubadilishana uzoefu na mataifa mengine ‘Exchange Program’ ili kuwajengea uwezo wataalam wa ndani.

“Kuna umuhimu kwa wenye viwanda kutoa fursa kwa vijana wa vyuo kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye viwanda vyao ili wapate ujuzi.”amesisitiza Dkt. Kiruswa.

Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi hususan katika sekta ya viwanda vya bidhaa za migodini.

Pia, amesema kuwa, Jukwaa hilo la Ushirikishwaji wa Watanzania lenye kauli mbiu ‘Uwekezaji wa Viwanda vya Uzalishaji wa Bidhaa za Migodini kwa Maendeleo Endelevu’ ni muhimu kwa wadau wa Sekta ya Madini kulitumia kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea uwekezaji.

“Ni matumaini yangu kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa suala la ushirikishwaji wa watanzania kwa wamiliki wa leseni na watoa huduma katika Sekta ya Madini nchini,”amesema Dkt. Kiruswa

Awali, akizungumza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa jumla ya mada saba zimewasilishwa katika jukwaa hilo lililoanza rasmi Mei 22, 2024 ambapo siku ya kwanza ziliwasilishwa mada mbili, siku ya pili zikawasilishwa mada sita na leo imewasilishwa mada moja.

“Mada zote lengo ni uchechemuzi wa kuanzishwa viwanda hapa nchini na bidhaa zote zinazohitajika migodini zipatikane hapa hapa nchini, Tunaposema kuna ongezeko la watanzania kupata fursa katika Sekta ya Madini ambalo kwa sasa limefikia asilimia 84 na miaka michache ijayo tutafikia asilimia 100 lakini ni fursa zipi tunazozifikia?”amehoji na kuongeza,

“Changamoto kubwa malighafi bado zinatoka nje ya nchi, fursa iliyopo sasa ni kujenga viwanda hapa hapa nchini, teknolojia za kisasa na bidhaa zinazotumika kwa wingi migodini zitoke hapa hapa nchini, serikali, watu binafsi tunawajibika kushirikiana ili kutimiza ajenda ya VISION 2030.

“Tunahitaji kuweka nguvu kubwa katika ‘Local Content na CSR ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na Sekta ya Madini,”amesisitiza Mhandisi Samamba.

Katika kongamano hilo, wadau mbali mbali wa Sekta ya Madini wamepewa tuzo na vyeti kutoka Tume ya Madini lengo ni kutambua mchango wao katika sekta hiyo.