January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa madini watakiwa kutambua dhamana yao

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewahimiza Watumishi wa Wizara ya Madini kutambua jukumu kubwa walilonalo katika kuwatumikia Watanzania kupitia Sekta hiyo muhimu ambayo ni miongoni mwa Sekta mhimili wa maendeo ya kiuchumi ya taifa na kuwataka kutambua nafasi zao kama viungo muhimu katika kufanikisha malengo ya Sekta hiyo.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Desemba 16, 2024 wakati wa kikao cha watumishi wa Wizara Makao Makuu kilichofanyika jijini Dodoma na kilicholenga kujadili na kufanya tathmini ya Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2024/25, kupokea ushauri, maoni na mapendekezo ya kuboresha shughuli za Wizara na Sekta kwa ujumla. Aidha, kikao hicho kimetumika kuwaaga na kuwapatia vyeti vya shukrani watumishi wa Wizara waliomaliza utumishi wao wa umma.

Amesisitiza uwepo wa vikao hivyo vya mara kwa mara vya watumishi wa Wizara na uongozi wa juu wa wizara na kueleza kwamba ni sehemu muhimu inayosaidia kuimarisha mahusiano kazini, kuongeza tija ya kazi pamoja na kupata nafasi ya kufanya tathmini ya majukumu, huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa watumishi kufanya mazoezi pamoja na kuzingatia ulaji wenye afya.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amewapongeza watumishi wa wizara waliostaafu utumishi wao wa umma na kutoa wito kwa watumishi wengine kujipanga vizuri pale utumishi wao unapokoma na kueleza kwamba, ‘’ kustaafu ni jambo linalohitaji kuweka mipango yetu vizuri ili maisha yetu yaendelee kuwa na furaha,’’.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi, Yahya Samamba amezungumzia madhumuni ya kikao hicho kwamba pamoja na masuala mengine kimelenga kufahamiana na amesisitiza Wizara kuyachukua maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na watumishi na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utendaji wa Wizara na maendeleo ya Sekta kwa ujumla.

‘’ Mhe. Naibu Waziri, tunakushuru wewe pamoja na Waziri ambapo miongozo na maelekezo yenu yanasaidia Wizara iende vizuri pamoja na usimamizi wa sekta hii. Tunakwenda nusu ya pili ya mwaka, tumeona ni vema tukakutana ili tuweze kufanya tathmini na kushauriana namnabora ya kuenndeleza sekta yetu na namna bora ya kuisimamia,’’ amesema Mhandisi Samamba.

Naye, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu, Issa Nchasi, akizungumza katika kikao hicho, ameshauri kuhusu wizara kutoa mafunzo kwa watumishi wanaotarajia kustaafu mapema ili kutoa nafasi kwao kujipanga vizuri kupitia mafunzo hayo kwa lengo la kuwasaidia kuweza kusimamia miradi yao na masuala mengine wanaotarajia kufanya pindi utumishi wao unapokoma.

‘’ Kustaafu si kubaya, jambo la msingi ni kujiandaa mapema na hapa Mhe. Mgeni rasmi nashauri watumishi wanaotarajia kustaafu wapewe mafunzo ya kustaafu mapema angalau miaka miwili au mitatu kabla ya kumaliza utumishi wao, hii itasaidia kuboresha masuala muhimu mapema,’’amesisitiza Nchasi.

Katika kikao hicho, watumishi wa kada zote wamepata nafasi ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo ya kuboresha utendaji kazi wa majukumu yao, Wizara na Sekta ya Madini