Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shindano la uzinduzi la Binti Afrika, litakalofanyika Machi 9, mwaka huu.
Zaidi ya warembo ishirini wako kwenye mazoezi makali kwenye Hoteli ya Kingazi Resort iliyopo Kijichi Mgeni Nani jijini Dar, kujiandaa na shindano hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni KL International Argency, Alfonce Mkama Ntare ambao ndio waandaaji wa kinyang’anyiro hicho amesema, maandalizi yote yameshakamilika na kinachosubiriwa siku hiyo ifike.
Mkurugenzi huyo amesema, lengo kubwa la shindano hilo ni kukuza lugha ya kiswahili pamoja na maadili ya kiafrika ambapo vigezo vyote hivyo vitazingatiwa katika kumpata mshindi.
Ameendelea kusema kuwa, shindano ambalo wengi hulifananisha na mashindano mengine ya mamiss lina utofauti mkubwa ambapo hili haliwatumii warembo waliokonda au wembamba kwakuwa kukonda au wembaba siyo kiwakirishi cha binti wa kiafrika.
“Hili ni shindano la mabinti wenye shepu zao za kiafrika haswa maana wengine wanalifananisha shindano hili na mashindano mengine ya mamiss ambayo huwakilishwa na warembo wembamba.
“Kwa kusema hayo naomba wananchi wajiandae kushuhudia shindano hilo linalotarajiwa kuleta mageuzi makubwa na kutoa ajira na kubadilisha maisha ya mabinti hao,” amesema.
Mkama alimalizia kwa kusema baada ya kinyang’anyiro cha uzinduzi, fainali yenyewe itakayowakutanisha mabinti kutoka mataifa mbalimbali Barani Afrika inatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kingazi Resort, Yeriko Asiphiwe Mahenge inayotumika kama kambi ya mabinti hao amesema, hoteli hiyo ina utulivu mzuri unaowafanya mabinti hao kuwa kambini kwa usalama na amani.
Amesema, mabinti hao wanatunzwa kwa huduma bora za vyakula, vinywaji na malazi safi.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wengine kufika hotelini hapo kujipatia huduma bora na ya kisasa inayokwenda na wakati.
More Stories
GETHSEMANE GROUP KINONDONI yaja na wimbo wa siku yetu kwaajili ya harusi
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA