Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaendelea kushirikiana na mamulaka za Upangaji, Umilikishaji na Upimaji ardhi kuhakikisha zinaendelea kutumia wataalumu wa fani ya sekta ya Ardhi ikiwemo wahitimu wapya ambao hawajaingia katika mfumo rasmi wa ajira hapa Nchini.
Akiongea wakati wa Mahafali ya 40 ya Chuo cha Ardhi Tabora, mapema jana mjini Tabora Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Mawendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amesema Wizara yake itaangalia uwezekano wa kutumia baadhi ya wahitimu hao katika zoezi la Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika mradi mkubwa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia utakaonza hivi karibuni katika Halmashauri 41 nchini.
Pamoja na kuwahaidi uwezekano huo Dkt. Kijazi amewata wahitimu hao kutambua kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira hapa nchini na kuwataka wahitimu hao kufikiria kuanzisha kampuni kwani serikali imekuwa ikishirikiana na kampuni binafsi hapa Nchini katika kazi mbalimbali za urasimishaji.
Aidha Dkt. Kijazi aliongeza kuwa bado kuna fursa kubwa katika sekta ya ardhi hapa Nchini jambo la msingi ni namna wahitimu hao wanavyoweza kuibua fursa hiyo akingeza kuwa ardhi iliyopangwa kupimwa na kumilikishwa ni asilimia 20 ya ardhi yote ya Tanzania.
Dkt. Kijazi ameagiza chuo cha Ardhi Tabora kuendelea kutoa ushauri kwa wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo na kuwa na kanzi data ya kuwatambua mahali waliko ili kuendelea kuwashauri hata baada ya kuwa wameingia katika soko la ajira kwa lengo la kuwashauri kuhusu fursa zilizopo.
Akijibu hoja za wanafunzi zilizojitokeza katika Risala yao kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Kijazi alisema baadhi ya hoja zao anazichukua kwa lengo la kuzifanyia kazi na baadhi yake kuzitolea maamuzi haraka iwezekenavyo.
Katika kuzitolea maamuzi baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wanachuo katika risala hiyo Katibu Mkuu Kijazi ameagiza chuo hicho kumpatia orodha ya vifaa vyanavyohitajika na vinavyoendana sayansi na teknolojia iliyopo ili elimu itakayotolewa chuoni hapo iendane na teknolojia ya kisasa.
Katika ziara yao kwa mgeni rasmi wahitimu hao walionesha kusikitishwa kwao na hutua ya Chuo Kikuu Ardhi kushindwa kuwadahili ili wajiunge na shahada katika chuo hicho pamoja kuwa wao ni wahitimu katika ngazi ya stashahada.
Akifafanua kuhusu hoja ya wahitimu hao Dkt. Kijazi amehaidi kwenda mbali zaidi ili kubaini ni kwanini wanafunzi hao wanakosa sifa za kuchaguliwa katika vyuo vikuu kwani kwa ufahamu wake wahitimu ngazi ya stashahada wanayo sifa ya kudahiliwa katika elimu ya juu.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa mabweni Dkt. Kijazi amewataka uongozi wa Chuo hicho kushirikina na Shirika la Nyumba la Taifa kutafuta eneo lingine ili waweze kujenga mabweni ya wanafunzi ikiwa ni hatua muhimu kukuza na kuendeleza Chuo hicho.
Awali katika Risala ya Raisi wa Wanafunzi chuoni hapo Bw.Alphonsi Makingi ilitaja mafanikio ya chuo hicho kuwa ni pamoja uwepo wa wahitimu wanaofanya kazi ya muda mfupi ya ubadilishaji taarifa za ardhi kutoka mfumo wa analojia Kwenda mfumo wa kidijiti inayotolewa na Wizara ya Ardhi hivi sasa.
Naye Profesa, Prof. Henry Mzale ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Ardhi Tabora aliyemwakilisha Mwenyeki wa Bodi ya Chuo hicho, aliwambia wahitimu hao kuwa furaha ya bodi yake itatokana na mafanikio ya chuo hicho kilichopo katika Manispaa ya Tabora.
Aidha mwanazuoni huyo alisema bodi yake inapongeza juhudi za chuo kwa kuwekeza katika kukuza miundombinu ya chuo ikiwemo ujenzi wa madarasa na jengo la maktaba chuoni hapo.
Prof. aliongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hii utawezesha wanafunzi kupata elimu na kupunguza baadhi ya changamoto zinazojitokeza na kuboresha taaluma chuoni hapo.
Aidha Prof. Mzale alibainisha kuwa juhudi kama hizi zitapelekea kuwepo kwa wanafunzi na kuongeza ufanisi kitaaluma.
Prof. Mzale ameshauri Wizara ya Ardhi kuhakikisha inawekeza katika mahabara ya uchoraji kwani ni moja ya nguzo ya mafunzo kwa vitendo kwa wanadfunzi hao na kuongeza kuwa ubora wa wahitimu unategemea ubora wa programu na vifaa vya kufundishia.
Katika hatua nyingine Prof. Mzale aliwakaribisha wahitimu hao kwenye ajira na utumishi uku akiwataka kuzingatia weledi na nidhamu vinginevyo wataishia kwenye utupu, lawama, na manunguniko.
“Kama ilivyo chunvi kwenye mboga ndivyo ilivyo kwa mwanadamu na nidhamu hivyo nawaasa kuacha tamaa ili msije mkatumbukia kwenye majanga.” Alionya Prof. Male.
Wanafunzi waliohitimu katika Chuo cha Ardhi Tabora ni astashahada na stashahda, katika fani zote zinazohusiana na sekta ya ardhi ikiwemo upimaji na ramani.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024