May 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Homera : Serikali yajipanga kuleta mageuzi sektabya sheria

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuleta mageuzi katika Sekta ya Sheria nchini.

Dkt. Homera Ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, yanayofanyika Jijini Arusha, amesema kuna umuhimu wa maboresho mbalimbali ya Kisheria kwakuwa Sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya 2050.

Amesema taifa linahitaji watu imara katika kusimamia sheria zitakazoleta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.” Kama mnavyofahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imeweka misingi yake katika sekta ya sheria ambayo ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu.

“Kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo ya kimkakati yakiwemo usimamizi wa mikataba ya ujenzi na manunuzi, Sheria za Anga na utatuzi wa migogoro ya anga, Sheria za kodi katika sekta ya Mafuta na Gesi, uendeshaji wa mashauri ya kodi, na Uendeshaji wa Mashauri katika Mabaraza mbalimbali ya Utoaji Haki,”amesema

Amesema mada zitakazo tolewa ni mahsusi kabisa katika kufikia lengo la Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake la maono ya Mageuzi katika Sekta ya Sheria.

Aidha Dkt. Homera amesema kuwa kuptia mafunzo haya Mawakili wa Serikali wataweza kushauri ipasavyo, kusimamia vizuri mashauri ya Serikali na kuwezesha Serikali Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufikia malengo yake ya Dira 2050.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika kuboresha utendaji kazi wao kwa viwango vya Kitaifa na Kimataifa.

Dkt. Possi amesema kuwa mafunzo hayo pamoja na kuongeza maarifa yatawasaidia Mawakili wa Serikali kulinda rasilimali za taifa, na kuwafanya mawakili hao kuwa kitovu cha umahiri katika kuratibu na kuendesha mashauri mbalimbali yanayofunguliwa dhidi ya Serikali.

“Tunatambua ili kulinda rasilimali za nchi na kwa ufanisi hatuhitaji tu Mawakili bali tunahitaji Jeshi la Kalamu lililosheheni maarifa ya kisasa, mbinu za usuluhishi za kidijitali na uwezo wa kuzuia migogoro kabla haijafika Mahakamani au kwenye Mabaraza ya Usuluhishi,”amesema Dkt. Possi.

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuendelea kuboresha ujuzi zaidi kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo.Maneno alieleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imeanza kufanya maboresho katika kuwaongezea ujuzi Mawakili wa Serikali katika masuala ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, ambapo mpaka sasa zaidi ya Mawakili wa Serikali 30 kutoka katika Ofisi hizi wamepata mafunzo na kuthibitishwa kuwa wataalamu kwenye maeneo ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Setka banafsi.

Mafunzo hayo ya Mawakili wa Serikali yanafanyika kwa siku tatu Jijini Arusha ambapo yameanza mei 18, 2026 na yanatarajia kuendelea hadi Mei 20, 2026.