January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DKT. Gwajima: Wasichana changamkieni ujuzi wa TEHAMA

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewasihi wasiachana kujitokeza kwa wingi kujifunza na kubobea kwenye ujuzi na maarifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwani kwa sasa tafiti zinaonesha asilimia 90 ya ajira kwa kipindi kijacho zitahiji ujuzi wa TEHAMA.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Aprili 28, 2022 jijiini Dar Es Salaam wakati akizindua wa pili Program ya Kuhamasisha Wasichana Barani Afrika kushiriki katika TEHAMA, Mpango ambao utawawezesha wasichana walio wengi kuwa na ushiriki mpana kwenye masuala ya teknolojia.

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa, kwa sasa Serikali ya Tanzania, imeridhia kutekeleza mikataba ya kimataifa na ya kikanda ikiwepo mkataba wa kutokomeza ubaguzi wa aina zote wa mwaka 1978, Azimio la Beijin la 1996, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa 1989, Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030, Ajenda ya Afrika tunayoitaka ya mwaka 2063 na Mkataba wa Afrika wa Haki ya Mtoto wa 1989.

“Mikataba hii na mingine ina lengo la kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia hivyo kama jamii ya watanzania, tunayokila sababu yakuweza kuyafikia malengo hayo kwakuzingatia muda uliowekwa” alisema Dkt. Gwajima

Akizungumza kwenye uzindunzi huo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema kama ilivyo kwa Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar wamekuwa wakitoa kipaumbele kwa watoto wa kike kupitia Programu ya Fawe na Femu lakini pia kupitia Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo kikuu cha Karume.

“Kama ilivyo kwa Tanzania Bara, tunachofanya kwa sasa nikuwawezesha wanawake wa vijijini kwenye Programu mbalimbali za Kisayansi ikiwepo ile ya kuwawezesha kutengeneza taa za umeme wa jua, hivyo mbali ya kujikita kwa kuangalia waliopo vyuoni vile vile kipaumbele tumekiweka pia kwa walio nje ya Vyuo” alisema Mhe. Riziki

Kwa upande wao mabinti Thereza Joseph wa Tanzania na Fatou Ndiaye kutoka Senegal waliokuwa wakisomea fani ya TEHAMA, wamepongeza juhudi zinazochululiwa kwa sasa katika nchi za kiafrika katika kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu na ujuzi mbalimbali.

“Mwanzoni sisi wakati tupo Sekondari tunajifunza kusuka mifumo wengi tulikuwa hatujua hatma yetu, lakini kutokana na msukumo huu unaowekwa na Serikali zetu tunaimani kabisa, utamwezesha Msichana kufikia malengo yake, maana kama unavyofahamu, jamii nyingi za kiafrika zilikuwa hazitoa kipaumbele kwa watoto wa kike kwenye suala elimu, lakini kwa muamko huu tunaiona kesho yetu” alisema Thereza kutoka Tanzania.

Akizungumza kwenye Uzinduzi huo, Lilian Mwamdanga Mkuu wa Idara ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, amesema Program hiyo itakwenda kufanyika katika mwaka wa fedha 2022/23, ambapo jumla ya Nchi 11 zitashiriki kwenye mpango huo zikiwepo Tanzania, Burundi, Mozambique, Niger, Mali, Kenya, Rwanda, DR Congo, Senegal, Uganda na Afrika Kusini

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima, akizungumza katika uzinduzi wa Programu ya kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika masuala ya TEHAMA uliofanyika jijini Dar Es Salaam leo tarehe 28/04/2022.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, akizungumza na waandishi wa Habari akielezea hatua zinazochukuliwa kwa upande wa Zanzibar kuwawezesha watoto wa kike katika masuala ya TEHAMA mara baada ya Uzinduzi wa Programu ya kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika masuala ya TEHAMA.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima akizindua Program ya Kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika TAHEMA Awamu ya Pili uliofanyika leo tarehe 28/04/2022 jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa msichana aliyenufaika na Program ya Kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika TAHEMA Awamu ya Pili Bi. Thereza Joseph kutoka Tanzania, akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya Uzinduzi wa Programu ya kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika masuala ya TEHAMA Awamu ya Pili uliofanyika leo tarehe 28/04/2022 jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima, (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wadau mbali mbali mara baada ya Uzinduzi wa Programu ya kuwawezesha Wasichana wa Kiafrika katika masuala ya TEHAMA Awamu ya Pili uliofanyika leo tarehe 28/04/2022 jijini Dar es Salaam.