Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametatua kero sugu iliyodumu muda mrefu inayowahusu ndugu wanaouguza wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam wakilalamikia uamuzi wa uongozi kuruhusu ndugu mmoja tu kwa wagonjwa wote kuingia kumuona mgonjwa wao hata wenye uhitaji wa ndugu wawili kulingana na hali ya mgonjwa.
Ametatua kero wakati akijibu malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana Jijini Dar es salaam katika mwendelezo wa ziara zake za kuhamasisha watumishi wa umma kuweka mikakati ya kuzungumza na wateja kila siku kwa lengo la kuboresha huduma kwa jamii kufuatia utekelezaji wa maelekezo yake kuwa kila kituo cha utoaji wa huduma za Afya hapa nchini kihakikishe kinaanzisha ‘saa ya kigoda cha sema na mteja boresha huduma’.
Aidha Dkt.Gwajima amewataka watumishi wa umma kubadilisha mfumo wa utendaji kazi uwe wenye vishawishi kwa wateja ili wavutiwe kufuata huduma zinazotolewa kama sehemu ya kujiandaa na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote
Kwa upande mwingine Dkt Gwajima ameelekeza kuwa, viongozi watoke maofisini wazungumze na wateja na wagonjwa ili wapate mitazamo yao kuhusu huduma kuwa wapi ziboreshwe. Waepuke kukaa ofisini na kupanga mipango kwa kusubiri kuletewa taarifa mezani kwani mara nyingi hazina uhalisia hali inayosababisha kichelewesha huduma bora kwa jamii.
Mganga mkuu wa Hospital ya Rufaa Mkoa wa Amana Dkt Bryson Kiwelu amesema hospitali ya amana imeanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa huduma kwa wagonjwa hali iliyosaidia mapato kuongezeka kutoka wastani wa shingi milioni 291 kwa mwezi hadi kufikia shilingi milioni 383 kwa mwezi hali iliyosaidia upatikanaji wa Dawa kwa asilimia 97.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa