January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Dugange aiagiza TSC kuchunguza sababu ya utoro kwa walimu

Na Joyce Kasiki,Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange ameiagiza Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC) kutafuta sababu ya walimu kufanya kosa la utoro ka kujirudia rudia na kisha kuchukua hatua ya kuitatua changamoto hiyo.

 Dkt.Dugange ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa siku moja wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu uliofanyika jijini Dodoma.

“Kama ambavyo nimetaarifiwa hapa,kosa la utoro kwa walimi linaonekana kuongoza kwa asilimia 66.5 ,na limekuwa likijirudia rudia kila mwaka,lazima viongozi wa TSC mlichunguze hili ili kujua kwa nini linatokea na kisha mchukue hatua ya kulitatua ili kulimaliza.”alisema Dkt.Dugange.

Aidha Dkt.Dugange amekemea tabia ya baadhi ya walimu wanaofanya shughuli zisizo za ualimu na mwisho wa siku wanaidhalilisha fani hiyo.

“Naiagiza Mamlaka ya nidhamu ya TSC kuchukua hatua mara inapojitokeza utovu wa nidhamu kwa walimu ili kuhakikisha wanakaa katika mstari na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yanayowaongoza kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu.”alisema Niabu Waziri huyo

Dkt.Dugange amezungumzia kuhusu namna serikali inavyoshughulikia changamoto za walimu ambapo alisema,Serikali inalifanyia kazi ili ziweze kutatuliwa.

Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuendelea kuajiri walimu,kupandisha vyeo pamoja na kulipa stahiki zao.

Mbali na hilo aliwataka kuendelea kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu katika mikoa yote huku akiagiza kupeleka vifaa vya TEHAMA katika mikoa minne ambayo imefanyiwa majaribio.

Naye Katibu TSC Paulina Mkwama waliokidhi vigezo alisema,TSC imekuwa na mafanikio lukuki huku akiishukuru Serikali kwa kuchangia katika mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya kitumishi wa walimu ikiwa ni pamoja na kuajiri ,kusajili walimu,kuthibitisha kazini walimu waliokidhi vigezo.

Aidha alisema,TSC wanajitahidi kusimamia makosa mbalimbali yakiwemo ya nidhamu ambapo alisema walimu wamekutwa na makosa 11,366 ambapo kati ya hayo kosa la utoro limeongoza kwa kuwa na asilimia 66.5.