📌 Mwananchi Communications Ltd yapongezwa kwa ubunifu
📌 Kongamano la Wajasiriamali wadogo na wa kati kuibua fursa (MSMEs)
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetoa mikopo ya shilingi bilioni 108.43 ili kuwezesha uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na mifugo nchini.
Hayo yamebainishwa leo Julai 5, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akifungua Kongamano la Wadau na Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (MSMEs) lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited na Kufanyika Jijini Dar es Salaam.
Amesema mikopo hiyo imetolewa hadi kufikia Machi, mwaka huu.
“Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38. zilitolewa kwa ajili ya uwekezaji na shilingi bilioni 70.427 zilitolewa kwa ajili ya kuendesha. Uwekezaji huo umeendelea kuwahakikishia masoko ya uhakika wakulima, wafugaji na wavuvi nchini,” amesema Dkt. Biteko
Amesema, mwaka 2023/24, Serikali kupitia Mfuko wa Wajasiriamali Wananchi (NEDF) unaotekelezwa na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) iliweza kutoa jumla ya mikopo 956 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 kwa riba ya asilimia 9. Asilimia 51 ya mikopo hiyo ilitolewa kwa wanawake na asilimia 28 ilitolewa kwa miradi ya vijijini.
Aidha, kupitia programu ya SANVN (SIDO, Azania Bank, NSSF, VETA na NEEC) inayotoa mikopo kwa ajili ya uwezeshaji viwanda kwa wajasiriamali wadogo (Shilingi milioni 8 hadi milioni 50) na wajasiriamali wa kati (Shilingi millioni 50 hadi milioni 500), mikopo 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 ilitolewa kwa Wanufaika wa SIDO kupitia Azania Benki na kutengeneza ajira 103 katika mwaka 2023/2024.
Ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Wajasiriamali wadogo na wa Kati (MSMEs) ili kuboresha, kukuza na kuendeleza biashara zinazochipukia kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Aidha, kongamano litaongeza fursa mbalimbali za kuwainua Wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs) ambao wanajadili kuhusu namna ya kuboresha, na kuendeleza ujuzi na hatimaye kukuza biashara ndogo na za kati kama ilivyo katika malengo yetu.
Pia, ameipongeza Mwananchi kwa kuwa na program habari na makala mbalimbali zenye kulenga kuboresha, kuendeleza ujuzi na kukuza biashara ndogo na za kati kama isemavyo,” amesema Dkt. Biteko.
“Tunauona umuhimu wa kampuni zote hizi kwa mchango tunaopata katika kuwezesha kusaidia maendeleo endelevu yenye uwiano katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kutengeneza fursa za uwekezaji, kukuza ajira na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amesema takwimu zinaonyesha asilimia 90 ya biashara zote Duniani ni ndogo na za Kati (MSMEs) ambazo zinachangia zaidi ya asilimia 50 ya ajira na zinachangia mpaka asilimia 40 ya Pato la Taifa la Uchumi unaokua. Pia takwimu hizo zinaongezeka pale unapohusisha biashara ndogo zisizorasmi.
“Kwa pamoja tushirikishane fursa, na namna ya kushughulikia changamoto, na kupanga mikakati bora kwa maendeleo endelevu ya uchumi wetu,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amewapongeza Mwananchi Communications Ltd kwa kuandaa kongamano hilo ili kujadili changamoto na namna ya kutatua changamoto hizo na kutumia fursa zilizopo katika Sekta ya Viwanda hususan katika ukuzaji wa uchumi na kuongeza kuwa Sekta hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kwa kutoa ajira kwa Watanzania
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu amesema kuwa chombo hicho kina mujibu wa kuchochea maendeleo endelevu nchini kupitia kongamano hilo.
More Stories
‘Valentine day’kutumika kutangaza mapango ya Amboni
Mashirikisho yaunga mkono azimio mkutano mkuu CCM
Watumishi wa Mahakama waonywa