January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko atoa maelekezo mpango wa kukabiliana na El Nino

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa maelekezo mbalimbali yatakayoboresha ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) mnamo Agosti 24, 2023.

Ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 13, 2023 jijini Dodoma wakati akizindua Mpango huo na kuugawa kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wa baadhi ya Taasisi za Serikali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.

Dkt. Biteto amesema Mpango huo umeandaliwa ili kuhakikisha kuwa Serikaii, wadau na jamii wanachukua hatua stahiki za kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na El Nino na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali ya madhara yatakayojitokeza.

“Ili kuwa na ufanisi katika kutekeleza Mpango huu, nazielekeza sekta zote kuchukua hatua kuainisha na kuandaa rasilimali za kuzuia na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake, kutambua maeneo hatarishi yenye viashiria vya kuathirika na maafa na kuandaa mpango wa kuzuia madhara na kukabiliana na maafa, kuelimisha wananchi na kuwahimiza kuhama kwenye maeneo hatarishi, umuhimu wa kuweka akiba ya chakula na kulima mazao yanayohitaji maji mengi pamoja na hatua za kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha yao na mali”, amesema Biteko.

Maelekezo mengine ni kuandaa na kutekeleza mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea, Idara ya Taasisi zinazohusika na mazingira, miundombinu, kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote, kuimarisha na kusafisha mitaro na makalavati, Sekta za Maji, Umeme na Mawasiliano ziweke mipango ya kuzuia madhara na kuhakikisha uharibifu katika huduma hizo unapewa ufumbuzi mapema, kutoa taarifa haraka kwa Mamlaka husika pale inapotokea maafa kwenye sekta na kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya maokozi na huduma za dharura pamoja na kutoa elimu kwa Watendaji katika ngazi zote ili wachukue hatua stahiki za kuzuia na kupunguza madhara ya El Nino yanayoweza kujitokeza.

Vile vile, amezitaka Sekta kuimarisha na kusafisha njia za maji ya mvua na maji taka pamoja na usimamizi wa taka ngumu na uwepo wa madampo, kuimarisha madaraja na kingo za mito na mabwawa katika maeneo yote ya kimkakati, kusimamia matumizi sahihi ya mitaro na njia za maji kwa kuzuia viwanda kutiririsha uchafu katika maeneo ya makazi na sehemu za kuzalishia maji, Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote ziandae mipango ya utekelezaji katika maeneo yao kwa kuzingatia mpango huu ulioandaliwa na kuhakikisha mvua hizi zinatumika kwa shughuli za maendeleo.

Pia, kufuatilia na kutekeleza maelekezo ya kitaalam pamoja na taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini na kuweka utaratibu wa kuandaa ujumbe mfupi na kuusambaza kwa njia ya simu. Aidha, ametoa msisitizo kuwa wizara zichukue wajibu wake wa kuandaa kukutana na wadau na watu walio chini yenu kuwapa maelekezo hayo na kwenye matangazo na hotuba zao kutenga eneo la kuweka ujumbe unaohusiana na kuwatahadharisha Watanzania juu ya uwepo wa madhara ya El Nino.

Akizungumza kuhusu Mpango huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa mara tu taarifa ya awali ya dalili za uwezekano wa uwepo wa El Nino ulipotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Ofisi ya Waziri Mkuu imetekeleza na kuratibu hatua kadhaa za kimsingi na za awali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawasilisha taarifa kwenye wizara na mikoa hasa mikoa husika ili kufanya tathmini ya maeneo yanayoweza kuathirika na kuandaa mipango ya hatua za kuzuia au kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini. Ameeleza kuwa, matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanaendelea kuongezeka ni pamoja na mvua kubwa za muda mfupi, joto kali, upepo mkali na vimbunga ambapo tathmini ya karibuni inaonesha matukio ya El Nino yataongezeka kwa idadi na ukubwa kadri ambavyo joto la dunia linaendelea kuongezeka.

“Mwelekeo wa mvua za vuli kwa mwaka 2023 unaonesha msimu wa mvua za vuli utachagizwa na uwepo wa El Nino, tunaendelea kufanya kazi masaa 24 kufuatilia mabadiliko katika bahari zote ambapo tunachokiona kwa sasa ni ukubwa wa El Nino kuwa katika nyuzi joto 1.2 ambao ni ukubwa wa wastani, na tunatarajia mvua hizo zitaenda mpaka mwezi Januari.” Amemalizia Dkt. Chang’a.