Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko ameipongeza taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuendelea kuandaa mbio za CRDB Bank Marathon, ambazo zimejielekeza katika kusaidia jitihada za serikali kuboresha sekta ya afya, kusaidia wenye uhitaji, pamoja na kukuza ustawi wa jamii.
Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo wakati wa kilele cha msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon ambapo Shilingi Milioni 350 zilikusanywa kwa ajili ya kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na uwezeshaji wa vijana.
“Niwapongeze kwa kuendelea kusaidia matibabu ya wakinamama na watoto wetu. Wakinamama ndio wamebeba uchumi wa Taifa letu. Lakini pia wakinama ndio waangalizi wa familia zetu hususani watoto. Hivyo ukiimarisha afya ya mama na watoto umeimarisha afya ya Taifa,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, alisema Serikali na Watanzania wanaona jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation.
Naye Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema CRDB Bank Marathon imesaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ari ya michezo nchini.
Dkt. Ndumbaro alisema mbio hizo zimekuwa jukwaa muhimu kwa wanariadha nchini kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la kimataifa kwani mbio hizo zimesajiliwa kimataifa na Shirikisho la Upimaji Mbio Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletic).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema katika kiasi cha fedha kilichokusanywa; shilingi milioni 100 zitakwenda kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Shilingi Milioni 100 kusaidia huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na Shilingi Milioni 150 uwezeshaji wa vijana.
Katika mbio hizo zawadi za jumla ya Shilingi Milioni 98.7 zilitolewa kwa washindi 60 wa mbio za kilometa 42, 21, 10, 5, pamoja na mbio za baiskeli za kilometa 65.
Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba alisema jumla ya washiriki waliojiandikisha mwaka huu ni 8,000 huku akisema lengo la mwaka kesho ni kupata washiriki 10,000 Tanzania, huku malengo ya washiriki Burundi na DRC wakiwa ni 3,000 kila nchi.
Mbio hizi zilizofanyika jijini Dar es Salaam, ni za tatu baada ya zile zilizofanyika nchini DRC, na Burundi. Nchini DRC mbio hizo zilifanyika tarehe 4 Agosti ambapo Dola za Marekani 50,000 zilikusanywa kusaidia kuboresha huduma za afya kwa watoto hospitali ya Jason Sendwe jijini Lubumbashi.
Kwa upande wa nchini Burundi, mbio hizo zilifanyika tarehe 11 Agosti ambapo Faranga za Burundi Milioni 120 zilikusanywa kusaidia wahanga wa mafuriko mkoa wa Gatumba jijini Bujumbura.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa aliwapongeza washindi wa mbio hizo, na kuwashukuru washirika wa mbio hizo wakiwemo kampuni za bima Sanlam na Alliance Life ambao ni washirika wakuu wa mbio hizo.
“Tunawashukuru sana washirika wetu na wakimbiaji wote kwa kuungana nasi katika juhudi za kusambaza tabasamu kwa watoto walioathirika,” alisema Mwambapa.
Washindi wa mbio hizo Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Moses Nengichi kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Sara Makera kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Hamida Nasor kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Mao Hindo Ako kutoka Tanzania.
Sara Makera mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake alieleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT.
“Mimi kama mwanamke ninajisikia faraja kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Watu wanapaswa kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoro na wakinamama pia hawastahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuunganisha pamoja katika juhudi hizi,” alisema.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa