Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko ameanza ziara ya kikazi katika jimbo hilo lililoko mkoani Geita.
Hiyo ni ziara ya kwanza kufanyika tokea ateuliwe na kuapishwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Mara baada ya kuwasili katika Jimbo hilo 24 Septemba 24, mwaka huu, Dkt.Biteko alipokelewa na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na viongozi mbalimbali.
Akizugumza katika Mkutano wa hadhara, Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kuona kuwa anaweza kumsaidia katika majukumu aliyokabidhiwa na kuahidi kuwa, atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwatumikia wananchi ili kuitendea haki imani iliyooneshwa kwake.
Amesema, chini ya uongozi wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kila kitu kilichopangwa kufanyika kinaendelea kufanyika kutokana fedha anazotoa katika miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo mradi wa umeme wa
Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa ndege, madarasa, vituo vya afya, utalii n.k.
Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka watendaji na watumishi nchini kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali kwani fedha hizo ndizo zinategemewa na watanzania katika kuwaletea maendeleo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini Dkt. Doto
Biteko katika nafasi hiyo kubwa na adhimu na kwamba wana imani kuwa ataitendea haki nafasi hiyo kutokana na historia yake ya uchapakazi na uadilifu.
Viongozi hao wakiwemo Wabunge na Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Geita wamemshukuru Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara wilayani Chato, ujenzi wa Chuo
cha VETA wilayani Nyang’hwale na upelekaji umeme vijijini katika vijiji vya Mkoa huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi zilizofanywa na Dkt.Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini na kueleleza kuwa amesaidia kuinua mchango sekta ya madini katika uchumi
wa nchi.
Ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi, ili wachimbaji
wachimbe madini kwa uhakika na kuongeza mapato ya nchi.
Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa, hatalifanyia mzaha suala la utoroshaji wa madini nchini na kwamba wote watakaotorosha madini watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanakosesha nchi mapato.
kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na umeme katika Mkoa Geita.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja