January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Angeline: Takwimu za sensa zitasaidia serikali kutatua migogoro ya Ardhi

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Ili kupunguza migogoro ya ardhi inayoweza kuepukika nchini,wito umetolewa Kwa wananchi kutoa taarifa sahihi za makazi na umiliki wake wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agousti 23,mwaka huu.

Ambapo mpaka sasa takribani siku 16 hili sensa ya 6 ifanyike nchini tangu taifa lipate uhuru ambapo kwa mara ya kwanza itafanyika na sensa ya makazi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula wakati wa zoezi la ufungaji wa makambi katika kanisa la Wasabato SDA lililopo Pasiansi Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Ambapo ameeleza kuwa takwimu zitakazopatikana kutokana na zoezi la sensa zitasaidia Serikali kuzuia na kutatua migogoro inayohusu ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza bila sababu za msingi ikiwemo ile ya umiliki wa zaidi ya mtu mmoja.

“Mhakikishe mnatoa taarifa sahihi za sensa ya makazi tukifanya hivyo tutaondoa migogoro isiyokuwa ya lazima katika sekta ya ardhi,” ameeleza Dkt.Angeline.Pia ametumia fursa hiyo kuwasisitiza.

Aidha Mhe Dkt Mabula amewasisitiza waumini wa kanisa hilo kujibu maswali ya sensa watakayoulizwa na makarani wa sensa kwani kwa kufanya hivyo ni takwa la kisheria.

Kwa upande wake Katibu wa Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania kanisa la Wasabato, Mchungaji David Makoye Maduhu,ameeleza kuwa kanisa linaridhishwa na kasi ya utekelezaji washughuli za maendeleo.

Huku akishukuru kwa uwepo wa ulinzi na usalama kwani tangu kuanza kwa makambi hayo nchi nzima hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani lilijitokeza wala kuripotiwa.

Katibu wa Jimbo la Nyanza kusini wa kanisa la Wasabato Mchungaji Nikodemas Ntabiudi, amempongeza Dkt. Angeline Mabula kwa juhudi zake za kuwatumikia wananchi wa Jimbo lake licha ya kuwa na majukumu mengine ya kitaifa pamoja na ushirikiano anaoutoa kwa kanisa la wasabato kila wanapomuhitaji.

Waumini wa kanisa la Sabato kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza walioshiriki makambi katika kanisa la Sabato Pasiansi wilayani Ilemela mkoani Mwanza.(Picha Judith Ferdinand)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula akizungumza na waumini wa kanisa la Sabato Pasiansi hawapo pichani kuhusu umuhimu wa kushiriki sensa ya watu na makazi.(Picha na Judith Ferdinand)
Mchungaji David Makoye akimuombea Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula na viongozi wengine wa nchi.(Picha na Judith Ferdinand)
Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kanisa la Sabato Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)