Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Buzuruga ambalo ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha milioni 200 huku ujenzi ulipofikia hadi sasa kiasi cha milioni 50 kimetumika.
Hivyo kukamilika kwa ujenzi huo kutatatua changamoto ya Watu kulala wawili hadi watatu kwenye kitanda kimoja kutokana na ufinyu wa jengo la wodi ya wazazi lililopo kwa sasa.
Mbali na kuweka jiwe hilo pia Mbunge huyo Dkt.Angeline amezindua jengo la mama na mtoto zahanati ya Ilemela ambao umegharimu kiasi cha milioni 33.4.Sanjari na hayo amezindua jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Nyakato lililogharimu kiasi cha milioni 85.9.
Ambapo kati ya fedha hizo milioni 40 zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri huku Mbunge alichangia matofali 3000 yenye thamani ya milioni 3.6.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi,Dkt.Angeline amewapongeza wananchi kwa ushiriki wao katika miradi hiyo kwani kazi kubwa imefanyika.Dkt Angeline ameeleza kuwa siku zote wanapounganisha nguvu kazi mambo lazima yaende mbele ambapo kuna mkono wa wananchi,Mbunge na serikali.
Ameeleza kuwa ili chakula kiive lazima uwe na mafiga matatu na katika ujenzi huo wa majengo ya mama na mtoto wameenda na mafiga hayo matatu kwa maana ya wananchi,Mbunge na Halmashauri.
“Hayo ndio mambo Rais anataka,hataki maneno maneno vali kazi ifanyike,ndio maana ya maendeleo endelevu yanayotokana na sisi wenyewe kumiliki miradi tunayoletewa na ile ambayo tumeshiriki,tulichofanya leo hapa kiwe muendelezo katika miradi yetu,”ameeleza Dkt.Angeline.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary, ameeleza kuwa ujenzi wa jengo jipya la wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Buzuruga hadi sasa umefikia hatua ya boma.
Mhandisi Modest kuwa kupitia chanzo cha mapato ya ndani Manispaa ya Ilemela imetoa milioni 72. 4 kwa ajili ya kukamilisha majengo mawili ya mama na mtoto katika zahanati za Ilemela na Nyakato ambazo zilikuwa zimekaa kwa muda mrefu bila kukamilika.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano