January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Angeline atoa vifaa kwa CCM Wilaya ya Ilemela

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula ametoa vifaa mbalimbali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela,ili kuimarisha chama hicho pamoja na kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama unaenda vizuri.

Dkt Angeline ametoa vifaa kwa ajili ya zoezi la uchaguzi wa viongozi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa Wilaya hiyo vyenye thamani ya zaidi ya milioni 12(12,848,000) ikiwemo Ream 582 zenye thamani ya shilingi 8,148,000, Kalamu boksi 20 zenye thamani ya shilingi 260,000.

Pia ametoa vifaa vingine kwa ajili ya kuimarisha chama kama ikiwemo luninga mbili kwa makada wa vijiwe vya Kahawa vya Kata ya Kirumba na Mwigulu Kawekamo vyenye thamani ya shiling 630,000, bati 22 kwa ajili ya kupaua ofisi ya CCM Kata ya Kahama zenye thamani 480,000,gharama za usafiri kwa Wakurugenzi wa uchaguzi wa Kata 19,matawi 126 na jumuiya zao jumla milioni 3.33(3,330,000).

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Dkt. Angeline amesema ameamua kutekeleza zoezi hilo kama sehemu ya wajibu wake kwa chama hicho pamoja na kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa CCM taifa na Samia Suluhu Hassan katika kuwarahisishia watendaji wa chama hicho kutekeleza zoezi la uchaguzi kwa amani, haki na uhuru

“Ni wajibu wangu kuwezesha vitendea kazi vya uchaguzi kwa matawi, kata na hata Wilaya, tunajua kuwa si matawi yote au kata zote zenye uwezo wa kugharamia shughuli zote za uchaguzi,”amesema Dkt.Angeline.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson Meshack amempongeza Mbunge huyo Kwa jitihada zake za kusaidia chama huku akiwataka viongozi waliopokea vifaa hivyo kuvitumia kama ilivyokusudiwa

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela Aziza Isimbula amewasisitiza watendaji wa chama hicho kwa ngazi ya kata na matawi kuhakikisha wanawasilisha taarifa za zoezi la uchaguzi katika maeneo yao kila siku linapokamilika

Katibu wa UVCCM Kata ya Kahama Cosmas Lutebeka,amemshukuru Mbunge huyo kwa kusaidia mabati yatakayotumika kukamilisha ofisi yao iliyokwama kwa muda mrefu.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula Akizungumza na baadhi ya wanachama wa CCM Wilaya ya Ilemela mara baada ya kutoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha chama hicho pamoja na kusaidia katika uchaguzi ndani ya chama hicho.picha na Judith Ferdinand
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula kushoto akimkabidhi Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson Mesha ream,ambayo ni moja ya vifaa alivyovitoa mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha chama hicho pamoja na kusaidia katika uchaguzi ndani ya chama hicho.picha na Judith Ferdinand
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula kushoto akiwakabidhi baadhi ya wanachama wa CCM vifaa alivyovitoa mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha chama hicho pamoja na kusaidia katika uchaguzi ndani ya chama hicho.picha na Judith Ferdinand