Na Eleuteri Mangi, TimesMajira Online, Morogoro
UJENZI wa Reli ya ya Kisasa (SGR) nchini unalenga kuleta maendeleo ya watu kwa kurahisisha muda wa usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo, ambapo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakuwa masaa matatu au dakika 90, hatua itakayopunguza muda mwingi kuupotea barabarani ili kuwahi kufanyakazi nyingine za maendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema hayo alipokuwa Ihumwa jijini Dodoma wakati anawaaga Menejimenti ya Wizara hiyo kuanza ziara ya kutembelea mradi wa SGR ili kujionea maendeleo yake.
“Wizara ya Habari ni Wizara muhimu sana katika nchi yetu na mradi huu pia. Ndiyo wizara yenye dhamana na habari kwa maana hiyo tumekuwa tukiutangaza sana, na kuulinda mradi huu ili kuwaonesha watanzania nini kinaendelea kwenye huu mradi” amesema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema, Tanzania ipo makini kuwekeza kwenye mambo ambayo ni muhimu katika kuleta manufaa na maendeleo ya watu na kusisitiza kuwa ni utamaduni mpya kwenye nchi yetu kuwa na taifa la wachapakazi, kuwa watanzania wanaojiamini na kuwa watu wanaopenda mambo mazuri ambayo yanaletwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi wake.
“Tunaposema huu ujenzi wa reli ni kitu, reli ya SGR ni kitu kinachokwenda kuleta maendeleo ya watu. Utakapoweza kusafiri kwa saa tatu au dakika 90 Dar es Salaam hadi Morogoro umepunguza muda mwingi wa kupoteza barabarani na kuwahi kwenda kufanyakazi,” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Mradi huo ni moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali nchini na kuwa miongoni mwa miradi mikubwa Afrika ambapo Serikali imewekeza trakriban trilioni saba (07) kwa kipande cha Dar es Salaam, Morogoro hadi Mkutupora mkoani Singida ambapo kipande cha Morogoro hadi Dodoma kimefikia asilimia 42 hadi kukamilika kwake.
Akitoa maelezo ya mradi huo kwa mwajumbe wa menejimenti ya wizara hiyo, Meneja wa mradi kipande cha Morogoro hadi Mkakutupora mkoani Singida Mhandisi Mteshi Tito amesema reli hiyo itatumiwa na treni ya abiria ambayo itakuwa na mwendo wa kasi ya kilometa 160 kwa saa na ya mizigo itatumia saa moja kwa kilometa 120 hatua inayopelekea mradi huo kuwekewa uzio kuanzia mwanzo hadi mwisho ili kuepusha muingiliano wa watu wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mhandisi Mteshi ameongeza kuwa, kipande cha reli ya SGR kati ya Morogoro na Mkutupora Singida kina jumla ya km 422 ambapo km 336 zinajumuisha njia kuu na km 86 sehemu za kupishania treni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema, Menejiment ya Wizara hiyo imeshuhudia na kujionea wenyewe uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali na kuongeza itakapokamilika reli hiyo kutakuwa na usafiri wa uhakika kutoka Dar es Salaam hadi Mkutupora Singida ambayo itakuwa na manufaa kiuchumi katika sekta ya usafirishaji.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba