November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DIB kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ya bima kwa faida ya wateja

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

BODI ya Bima ya Amana(DIB) imesema inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ya bima kwa ajili ya kukuza ukuaji wa sekta hiyo ili kuhakikisha sekta ya bima inafanya kazi kwa ufanisi na kwa faida ya wateja.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na  Gavana wa Benki kuu ya Tanzania(BoT)na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Wa bodi ya bima ya Amana Emmanuel Jutuba ameeleza kwenye maonesho ya wakulima  yanayoendelea Nzuguni kwenye uwanja wa Nanenane na kueleza kuwa majukumu ya bodi hiyo ni kukagua na kutoa leseni kwa kampuni za bima ili kuhakikisha zinafaa kuendesha shughuli za bima.

Amesena DIB inajukumu muhimu katika usimamizi na udhibiti wa sekta ya bima nchini hivyo Jutuba amesema bodi hiyo itaendelea kudhibiti , kusimamia na Kufuatilia  kampuni zote za bima kuhakikisha zinazingatia sheria na kanuni ili kuweka viwango vya maadili na kuimarisha uwazi katika utendaji wa kampuni za bima.

Ametaja majukumu mengine kuwa ni pamoja na kutathmini Malalamiko kwa kupokea na kuyatatua kutoka kwa wateja kuhusu huduma za bima.

“Natoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Bodi ya bima ya amana kujifunza zaidi, wanapaswa kuelewa kuwa tunaendeleza na kuboresha mazingira ya biashara ya bima kwa ajili ya kukuza ukuaji wa sekta hii ili kuhakikisha sekta ya bima inafanya kazi kwa ufanisi na kwa faida ya wateja, “alieleza.

“Sisi kama benki kuu tunaendelea kusimamia benki zisitetereke ambapo tupo katika mchakato wa kuboresha muundo wa kisheria na kiutendaji ili kuchangia kikamilifu na kwa kwa ubora na mchakato huu unalenga kuifanya Bodi ijitegemee kiutendaji, “alisisitiza Gavana huyo

Alieleza ukubwa wa mfuko huo kuwa hadi kufikia June 30,2023 Mfuko wa bima ya amana ulikuwa na shilingi Trilioni 1.04 ambazo zimetokana na mchango wa Serikali wa shilingi Bilioni 1.05 ambazo zilitolewa wakati wa kuanzisha mfuko mwaka 1994 na kufafanua kuwa hadi kufikia June 30,2024 mfuko ulikuwa na wanachama 44.

Mbali na hayo alieleza muundo wa Bodi hiyo kuwa upimo chini ya Mamlaka ya Bodi ya wakurugenzi ambayo ina jukumu la kuunda Sera na kuhakikisha utawala bora.

“Kwa mujibu wa Sheria iliyounda bodi ya bima ya amana, Bodi ya wakurugenzi ya bodi ya amana imejumuisha wajumbe wanaotoka BoT ambaye ni Gavana, Mwakilishi wa wizara ya fedha, Katibu Mkuu wizara ya fedha na Wajumbe wengine watatu wanaochaguliwa na Waziri wa fedha, “alisema