December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diallo awataka wakulima Ngara kutumia mbolea

Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo akizungumza katika kikao kifupi baina ya wajumbe wa bodi, Menejimenti ya TFRA na wajumbe wa Bodi ya Chama cha Wakulima Ngara kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Ngara.
Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo akiwa katika picha na menejimenti ya TFRA na Uongozi wa Bandari ya Rusumo wakati wa ziara ya kikazi Wilayani Ngara tarehe 13 Aprili, 2024

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo amewataka wakulima mkoani Kagera kujikita kwenye kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji kwenye mazao mbalimbali shambani.

Dkt. Diallo ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wakulima na mawakala wa usambazaji wa mbolea za ruzuku wilayani Ngara.

“Nia yetu kubwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wakulima kwa kuongeza uzalishaji baada ya kutumia mbolea zitakazopelekea kuongeza tija kwenye uzalishaji” Dkt. Diallo alikazia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amewataka wakulima kuwekeza zaidi kwenye kupima afya ya udongo ili waweze kutumia mbolea inayoendana na uhitaji wa udongo.

Amesema, matumizi sahihi ya mbolea yanaleta tija kwenye uzalishaji hivyo nakuwasihi wakulima kuendelea kutumia mbolea sahihi kulingana na uhitaji wa udongo wao baada ya kuupima.

Naye Kaimu Meneja wa Chama cha Wakulima Ngara, Fadhili Damian Kamhanda amesema Wilaya ya Ngara ilifanikiwa kupokea tani 65 za mbolea sawa na mifuko 1300 iliyosambazwa kwa wakulima kwa asilimia 98.

Amesema, chama chao kiliingia mkataba na kampuni za OCP na Minjingu ili kusambaza mbolea za ruzuku ambapo ni mara ya kwanza kwa mbolea kufikishwa wilayani humo.

Kwa upande wake Mkulima mnufaika wa mbolea za ruzuku, Fred Gahanga amesema amenufaika na mbolea za ruzuku na anategemea kufanya vizuri kwenye uzalishaji kwa msimu huu wa kilimo.

“Basi mimi nilijaribu tu kutumia mbolea kwenye ekari moja nikaona ni kweli ukitumia mbolea naweza kuvuna kuanzia kilo 30 hadi 35” Fredy amesisitiza