November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dhamira ya Rais Samia ni kuona wananchi wananufaika na miradi katika maeneo yao-Kapinga

📌 TPDC yatekeleza maagizo ya Dkt.Biteko Msimbati

📌 Wananchi kuanza kunufaika na uwepo wa kituo cha Afya na Polisi

📌 Kapinga asisitiza ushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Kapinga amesema hayo leo Septemba 09,2024 wilayani Mtwara Mkoa wa Mtwara wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyolenga kukagua visima vya kuzalisha Gesi Asilia katika eneo la Mnazi Bay pamoja na miradi inayofanyika kwa manufaa ya jamii kutokana na uwepo wa gesi hiyo (CSR) ikiwemo ujenzi wa kituo cha Afya na kituo cha Polisi katika eneo la Msimbati.

“Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaonesha kwa vitendo jinsi anavyowajali kwa kuhakikikisha mnapata huduma bora kupitia miradi hii.” Amesisitiza Kapinga

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ni kujionea thamani ya miradi hiyo ambayo itanufaisha wananchi wa Msimbati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko aliyoyatoa Novemba 15, 2024 mara baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Amesema ujenzi wa kituo cha Afya unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2024 huku ujenzi wa Kituo cha Polisi nao ukiwa ukingoni.

Kapinga amesisitiza kuwa, Serikali ipo pamoja na wananchi katika kuhakikisha inawapelekea maendeleo.

Katika hatua nyingine, Kapinga amewaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kwa kuanza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.