March 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DED Mweli:Tumeweka kipaumbele kusikiliza kero za wananchi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Mbarali

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imesema imeweka mkakati maalum wa kutoa kipaumbele kwa kuwapokea wananchi na kusikiliza kero zao wakati wowote bila kuweka urasimu au vikwazo.

Aidha, imeelezwa kuwa wananchi watapokelewa bila kulazimika kuwa na miadi maalum ili kumuona Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma na utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema mwananchi yeyote anayefika ofisini kwa Mkurugenzi atapokelewa na changamoto yake kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesema halmashauri pia imeweka utaratibu wa Mkurugenzi kuongoza timu ya wakuu wa idara na wataalamu kufanya ziara za kila wiki katika kata mbalimbali ndani ya wilaya hiyo.

Kupitia ziara hizo, timu hiyo hukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo miradi iliyoanza miaka ya nyuma na inayoendelea kutekelezwa pamoja na ile ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Mweli amesema jukumu la halmashauri ni kuhakikisha miradi yote inasimamiwa kikamilifu ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Baada ya ukaguzi wa miradi, viongozi hao hukutana na wananchi katika mikutano ya hadhara kwenye kata husika ili kusikiliza kero zao, hasa kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kufika makao makuu ya halmashauri.

“Katika mikutano hiyo tumekuwa tukisikiliza changamoto za wananchi, baadhi tunazijibu papo hapo na zile zinazohitaji ufuatiliaji zaidi tunazichukua na kuzirejesha majibu kupitia madiwani au watendaji wa kata husika,” amesema Mweli.

Aidha, amesema halmashauri imeanzisha kituo maalum cha kupokea na kusikiliza kero za wananchi kupitia simu, ambapo wananchi wanaweza kupiga simu na kuwasilisha changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi.

Amesema kero zinazowasilishwa hupokelewa na kufikishwa kwa wakuu wa idara husika, kisha kupelekwa kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya maamuzi na baadaye majibu kurejeshwa kwa mwananchi kupitia namba yake ya simu.

Mweli amesema pia kituo hicho kitakuwa na daftari maalum la kusajili kero zote zinazowasilishwa na wananchi ili kuweka kumbukumbu sahihi za taasisi kuhusu changamoto zinazopokelewa na hatua zinazochukuliwa.

Amesema kila wiki halmashauri hufanya kikao cha wakuu wa idara kujadili kero hizo na kufuatilia utekelezaji wake.

Kwa mujibu wa Mweli, kituo hicho kitasimamiwa na Idara ya Utawala na watumishi wa halmashauri watakuwa wakipokea simu za wananchi ndani ya muda wa kazi.

Amesema muda wa kupiga simu ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri, ingawa katika mazingira ya dharura wananchi wanaweza kuwasiliana kupitia namba binafsi za viongozi wa halmashauri, ikiwemo ya Mkurugenzi Mtendaji.

Mweli amesema lengo la utaratibu huo mpya ni kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kueleza changamoto zao na hatimaye kuondokana na kero zinazowakabili.

Aidha, amesema halmashauri imejikita pia kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo, kwani mara nyingi kero za wananchi hutokana na kuchelewa au kutokamilika kwa miradi.

“Hivi karibuni nilielekeza wataalamu wa Idara ya Ujenzi kufanya tathmini ya miradi yote viporo. Tathmini ya awali imeonesha kuwa takribani shilingi bilioni 2.5 zinahitajika ili kukamilisha miradi hiyo,” amesema.

Amesema halmashauri inapanga kutenga fedha hizo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora.

Kwa upande wake, Patrick Alfan mkazi wa Mawindi wilayani Mbarali, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho cha kusikiliza kero za wananchi kutakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni.

Amesema baadhi ya wananchi hushindwa kufika makao makuu ya wilaya kutokana na umbali na gharama za usafiri, hivyo uwepo wa kituo hicho utarahisisha kuwasilisha changamoto zao.

“Kuna changamoto nyingi wilayani hapa, lakini watu wengine wanaishi mbali na makao makuu ya wilaya hivyo gharama za kufika zinakuwa kubwa. Hatua hii ya kuanzisha kituo cha kupokea kero itakuwa msaada mkubwa,” amesema.