December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCEA yaongeza kasi udhibiti dawa za kulevya

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kuwafunda vijana wa rika mbalimbali nchini kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya ikiwa ni mwendelezo wa kampeni yake kwa jamii.

Akitoa elimu juzi kwenye hafla ya ufunguzi wa mashindano ya shule za sekondari (UMISSETA) Kitaifa, yanayoshirikisha walimu na wanafunzi zaidi ya 4000, Mjini Tabora, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka hiyo Kanda ya Kati Mzee Kasuwi ameeleza kuwa wanafunzi ni wahanga wakubwa wa dawa za kulevya.

Amefafanua kuwa wanafunzi walio wengi hushawishiwa kirahisi na wenzao hivyo kuingia katika mkumbo wa kutumia kilevi ikiwemo dawa za kulevya huku wengine wakijaribu hata kutumia gundi na petroli ambayo ni aina ya dawa hizo.

Amebainisha kuwa Mamlaka hiyo chini ya Usimamizi wa Kamishna Jenerali Aletas James Lyimo imejipanga vizuri kufikia makundi mengi zaidi ili kufanikisha kampeni hii ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya miongoni mwa jamii.

‘Kupitia kampeni hii, nawasihi walimu na wanafunzi wote tukatae kushawishiwa na mtu yeyote yule kuingia kwenye mtego wa biashara ya dawa za kulevya au kutumia dawa hizo, dawa za kulevya zinaharibu ndoto zenu’, amesema.

Kasuwi amesisitiza kuwa dawa hizo zina madhara makubwa kiafya, kiuchumi, kijamii, kimazingira na kisiasa, alifafanua baadhi ya madhara hayo kuwa ni kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, homa ya ini, kifua kikuu na kukosa maadili.

Madhara mengine ni kuongezeka kwa vitendo vya uharifu, ubakaji, wizi, uchafuzi mazingira, mfumuko wa bei, utakatishaji fedha, kupata viongozi wasio waadilifu, kusambaratisha familia na ukame utokanao na kuharibu vyanzo vya maji.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha kampeni hii inapata mafanikio makubwa miongoni mwa jamii wataendelea kuanzisha na kutumia Klabu za wapinga rushwa ambazo pia zitatumika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, huku akiwataka kutoa ya siri taarifa kwa kupiga simu ya bure namba 21.

Akifungua mashindano hayo Waziri wa Michezo Dkt Ndumbalo amesema kuwa michezo ni burudani, afya na ajira hivyo akawataka walimu, wazazi na walezi kusimamia ipasavyo mienedno ya watoto ili kunufaika na michezo hiyo.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika shule zote ikiwemo kumwaga mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.