Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online
MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Halima Bulembo amekabidhi hundi yenye thamani ya sh.milioni 136 za mikopo kwa vikundi 30 vya walemavu, vijana na wanawake wa wilaya hiyo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Akikabidhi hundi hiyo wilayani humo Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa, atakuwa mkali kwa vikundi ambavyo vitashindwa kurudisha marejesho ya fedha hizo kwa wakati ili kusaidia wengine waweze kukopa.
“Kundi la vijana ndio mmekuwa na changamoto katika urejeshwaji wa fedha za mikopo, hivyo niwaambie tu mimi ni DC kijana mwenzenu nitahakikisha nawafuatilia kwa ukaribu ili muweze kurejesha kwa wakati,”amesema DC huyo.
Bulembo amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha inawainua kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ambayo watakapoitumia vizuri itawasaidia kuondokana na umasikini.
Awali Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Muheza, Vije Mfaume amesema kuwa, wamefanikiwa kutoa asilimia 100 ya malengo ya mikopo hiyo waliyojiwekea ya kutoa kiasi cha sh.milioni 337.
“Katika kipindi cha mwaka 2020/21 tuliweza kupata marejesho ya fedha za mikopo kiasi cha shilingi milioni 151 kutoka katika vikundi 25 hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo,” amesema Mfaume.
Vije amesema, mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi vinavyojishughulisha na miradi mbalimbali ikiwemo usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia bodaboda, ufugaji wa kuku, kilimo cha mbogamboga, duka, karakana ya kuchomekea, mgahawa, biashara ya ununuzi na uuzaji wa viungo, ununuzi na uuzaji wa nafaka na ununuzi wa vifaa vya kuoshea magari.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halamshauri hiyo ya Muheza, Issa Msumari amesema kuwa, kwa mwaka 2020/21 jumla ya shilingi milioni 337,000,000 zimetolewa kwa vikundi 55 ambapo wanawake ni vikundi 27,(152,000,000), vijana ni vikundi 21 shilingi (152,000,000) na watu wenye ulemavu ni vikundi 7 (33,000,000).
Amesema, katika kipindi hiki halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya, shilingi 136,000,000 kwa vikundi 23 ikiwemo vikumdi 10 vya wanawake shilingi (5,500,000) vijana 9 shilingi (62,500,000) na watu wenye ulemavu 4 (22,000,000) vyenye jumla ya washiriki 179 wakiwemo wanawake 94 vijana 64 na watu wenye ulemavu 21.
Kaimu Mkurugenzi huyo ameiasa vikundi hivyo vilivyokabishiwa mikopo kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili watu wengeni wapate fursa ya kukopeshwa huku akiahidi kuwa mkali kwa vikundi vitakavyoshindwa kurejesha fedha hizo.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto