Na Suleiman Abeid, Times Majira Online, Shinyanga
WAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameonywa kuacha tabia ya kukata miti ovyo hali inayochangia uhabirifu wa mazingira katika Manispaa hiyo ambapo kuanzia sasa atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko wakati wa zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambalo limeandaliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.
Mboneko amesema kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu ye yote kukata mti ovyo na iwapo ana hitaji la kufanya hivyo atapaswa kufuata sheria kwa kuomba kibali kutoka mamlaka husika vinginevyo atakamatwa na kutozwa faini isiyopungua shilingi 50,000.
“Nimpongeze Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuunga mkono juhudi za upandaji miti katika wilaya yetu ya Shinyanga, lakini pia nivipongeze na vyombo vingine vya ulinzi ambavyo vimekuwa vikisapoti kampeni yetu ya upandaji miti katika wilaya ya Shinyanga,”
“Tunaendelea kuwasisitiza wananchi wetu wa Shinyanga waendelee kupanda miti hasa hii ya matunda, lakini nitoe angalizo katika maeneo yote ya wilaya yetu ni marufuku kukata miti bila kibali, na ni marufuku kupitisha mifugo mjini, kwanza inachafua mazingira na inakula miti yetu, ukikamatwa faini ni shilingi 50,000.00” ameeleza Mboneko.
Mkuu huyo wa wilaya amesema mtu ye yote anayetaka kukata mti lazima aombe kibali, hata kama ni Taasisi zenye kazi za ujenzi wahakikishe wanapata kibali kwanza kabla ya kukata miti na atakayekwenda kinyume na maelekezo ya Serikali sheria itachukua mkondo wake.
“Niwaombe viongozi wa mitaa na vijiji wahakikishe miti hii inayopandwa inalindwa ili iweze kukua vizuri, na hii ni pamoja na kutopitisha mifugo barabarani, miti hii inapandwa kwa gharama kubwa, lazima ilindwe wakati wote,”
“Tumepokea pia maelekezo ya mheshimiwa Makamu wa Rais, kuendelea kupanda miti milioni moja na laki tano kila mwaka, na sisi tutaendelea kufanya hivyo katika wilaya yetu ya Shinyanga kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa mazuri na tunaendelea kuyatunza, kila mmoja awe mlinzi wa miti hii inayopandwa,” ameeleza Mboneko.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amesema wameamua kupanda miti ikiwa ni katika kuunga mkono maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.Kamanda Magomi amesema Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limejipanga kupambana na mazingira na litaendelea kuwaunga mkono viongozi wakuu wa Serikali kwa kuhakikisha zoezi hilo la upandaji miti linakuwa endelevu.
“Kama alivyoongea Mkuu wa wilaya, Shinyanga ya kijani inawezekana, Shinyanga bila ukame inawezekana, Jeshi la Polisi tumejipanga kupambana na mazingira lakini tunaendelea kuwaunga mkono viongozi wetu kuhakikisha kuwa tunaendelea kupanda miti, na wale wote watakaokata miti bila kibali, tuko timamu kwa ajili ya kuwashughulikia,” ameeleza Magomi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga, Dkt. Luzila John amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuandaa zoezi la upandaji miti katika eneo la hospitali hiyo na kwamba kwa upande wao wamejiandaa kikamilifu kuilinda miti hiyo kuhakikisha inakua vizuri.
Naye Ofisa Mazingira katika Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga amesema hivi sasa pamoja na kupanda miti kwa ajili ya kivuli na kuhifadhi mazingira lakini pia wanahimiza suala la upandaji miti kwa ajili ya matunda.
“Leo hii Jeshi la Polisi limeshiriki katika zoezi la upandaji miti ikiwa ni utekelezaji wa lengo la kitaifa la kupanda miti milioni moja na laki tano, tuna changamoto nyingi nyote mnazijua, maji ni tatizo, umeme na kadhalika, kubwa sana ni mabadiliko ya tabia nchi,”
“Sasa ni vizuri tunapoipanda miti hii ya leo, miti elfu moja na mia mbili, tuweke alama ambayo ni ya kudumu, tusipande tu kwa sababu tumekuja na tunatakiwa kuondoka kwa muda, ni vizuri tupande miti michache ambayo itakuwa na uhakika wa kukua na kudumu,” ameeleza Manjerenga.
More Stories
Hoja ya Lusinde yawaibua wagombea Urais ,wajumbe washangilia
‘Ni Wasira ‘Makamu Mwenyekiti CCM Bara
15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe