December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Nyasa ataka wananchi kushirikiana ujenzi wa miradi

Na Netho Credo,TimesMajira Online. Nyasa

MKUU wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba, amewataka wananchi wilayani hapa kutatua changamoto kwa kushirikiana katika ujenzi wa miradi ya maendeleo bila kuisubiri Serikali.

Ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika shule mpya ya Sekondari Luhangarasi na kukabidhi cheti cha usajili kwa uongozi wa Kata ya Luhangarasi Tarafa ya Mpepo.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Isabela amewapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya madarasa manne, jengo la utawala na matundu nane ya vyoo yaliyotumia zaidi ya sh. Milioni 60, zilizochangwa na wananchi, kupitia Chama cha Ushirika cha Luhangarasi AMCOS kwa lengo la kutatua changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari katika Kata hiyo na kuwalazimu wanafunzi, kutembea umbali wa kilomita 9 kufuata sekondari kata jirani ya Kingerikiti.

Amesema wananchi wa Kata ya Luhangarasi ni mfano wa kuigwa katika Wilaya ya Nyasa kwa kuwa mara baada ya kuona wana tatizo la ukosefu wa shule ya sekondari, waliamua kushirikiana na kujenga shule yao kwa asilimia mia moja bila kuisubiri serikali.

Ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuiga mfano huo wa kujitatulia matatizo yao wenyewe, ili kujiletea maendeleo kwa haraka.

Awali akisoma taarifa ya shule hiyo Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata, Philemon Ngaponda amesema ujenzi huo ulianza mwaka 2019 kwa vikao halali na vilivyowashirikisha wananchi, wakakubali kutatua changamoto ya watoto wao kutembea umbali wa kilomita 9 kufuata shule, hali iliyokuwa ikiwapa usumbufu mkubwa kuweza kufuatilia maendeleo ya shule.

Nao wananchi hao wameupongeza uongozi wa Wilaya ya Nyasa kwa juhudi zao za kuhakikisha shule hiyo inapata namba ya usajili S.5524 Luhangarasi Sekondari na kuwapeleka wanafunzi kuanza masomo katika shule hiyo mwaka huu kwa wanafunzi 188 wa kidato cha kwanza kudahiliwa shuleni hapo.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nyasa, Mwalimu Rogers Semwalekwa amewapongeza wananchi hao kwa kutatua changamoto ya ukosefu wa shule na ameunga mkono halmashauri kwa kutoa vifaa vya kufundishia vyenye thamani ya sh. milioni 1.2.

Pia tayari shule imeingizwa kwenye mfumo wa malipo ya Pranrep kwa ajili ya kupewa fedha za ruzuku za elimu bila malipo kutoka serikalini na tayari akaunti ya shule imefunguliwa na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali shuleni hapo, ili kuunga mkono jitihada za wakazi wa Luhangarasi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Jimson Mhagama amewapongeza wananchi hao na kuwataka kuendeleza juhudi hizo ili kutatua changamoto nyingine na kuwaahidi serikali, inaendelea kushughulikia Utatuzi wa changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo.