December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Nkasi awa mbogo kwa waliovamia msitu uliohifadhiwa kisheria

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

MKUU wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Peter Lijualikali amewapiga marufuku watu waliovamia na kulima kwenye hifadhi ya msitu wa Mfili ambacho pia ni chanzo cha maji na kuwa yeyote atakayekutwa ndani ya hifadhi hiyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Agizo hilo amelitoa jana alipokuwa akizungumza na Wananchi wa eneo hilo na kusema kuwa serikali ilishatoa maagizo ya mtu yeyote asiingie ndani ya hifadhi hiyo ya Mfili na kufanya shughuli zozote za kiuchumi lakini ameshangaa kuona kwamba bado kuna watu wameingia ndani ya hifadhi hiyo na kulima.

Hivyo amesema kuwa kuanzia sasa ni marufuku kuingia ndani ya hifadhi hiyo ya msitu na kwa wale waliolima ndani ya hifadhi hiyo wahesabu kwamba wameingia hasara kwa maana hairuhusiwi kabisa kuingia ndani ya hifadhi hiyo na kuendelea na shughuli za  kilimo.

“”Ni marufuku kabisa kuendelea na shughuli ndani ya hifadhi hiyo na kwa wale waliolima wamefanya kosa na wamevunja sheria na kwa maana hiyo hesabuni hasara kwani sitaki kumuona mtu yeyote akiingia ndani ya hifadhi hiyo na kwenda kuhudumia mashamba yake na kama itabainika umeingia ndani ya hifadhi hiyo utakumbana na mkono wa sheria””,alisema

Na ameagiza eneo hilo kuendelea kuifadhiwa vizuri na siku chache zijazo itafanyika oparesheni maalumu ya kuwasaka wale wote wanaokaidi agizo hilo la serikali ambalo limelenga kuuhifadhi msitu huo ili kulinda chanzo cha maji cha Mfili kinachotegemewa na Watu wengi katika mji wa Namanyere.

Awali mwenyekiti wa kitongoji cha Nkomolo Stephen Tontololo alimuomba mkuu wa wilaya kuwaacha wale waliolima ndani ya hifadhi hiyo kwa muda ili waweze kuvuna mazao yao waliyoyalima baada ya hapo wasilime tena.

Ombi hilo la Mwenyekiti lilikataliwa na mkuu wa wilaya na kuwa hawezi kuruhusu sheria ivunjwe ili wavamizi wa msitu waendelee kufanya shughuli zao humo kwanza tu kitendo cha kulima wametenda kosa hivyo hawezi kuruhusu jambo hilo liendelee.

Msitu huo wa Mfili umehifadhiwa chini ya sheria za serikali za mitaa  ya usimamizi wa rasilimali za maji Namb 11  ya mwaka 2009 ambapo halmashauri kupitia baraza la Madiwani walitunga sheria ndogo ya kuuhifadhi msitu na chanzo hicho cha maji.

Mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali akizungumza na Wakazi wa Mfili juu ya kuondoka kwenye hifadhi hiyo ya msitu wa Mfili
Bango linaloonyesha kuwa eneo hilo limehifadhiwa kisheria.
Wananchi wa eneo la Mfili wakimsikiliza mkuu wa wilaya juu ya katazo la kuingia ndani ya hifadhi ya Mfili