December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo azindua zoezi la upimaji afya bure

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, jana Juni 24, 2024 amezindua rasmi zoezi la upimaji afya bila malipo katika viwanja vya Mnazi mmoja wilayani humo, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hiyo kujua afya zao.

Mpogolo amesema, huduma hiyo inayotolewa inayojulikana kama ‘afya check’ ni muhimu katika jamii, kwani inaonesha kuwajali wananchi katika mustakabali wa afya zao kulingana na hali zao kiuchumi.

Wakati akizindua huduma hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, ametoa shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika kufanikisha zoezi hilo la utoaji huduma ya afya, ikiwemo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inayotoa huduma ya saratani kwa jamii.

“Niwashukuru sana wale wote waliofanikisha zoezi hili kwani ni wazi kuwa, wadau hao wapo sambamba katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhudumia jamii, hivyo nitoe wito kwa wananchi wote hususani wa Jiji la Dar es Salaam kutumia fursa hii ili waweze kujua afya zao”, amesema Mpogolo.

Taasisi ya Saratani Ocean Road ni miongoni mwa Taasisi ambazo zimeshiriki katika zoezi hilo kwa kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa Saratani ya Matiti, saratani ya Mlango wa kizazi pamoja na Tezi dume kwa njia ya kupima damu bila malipo yoyote.

Aidha, huduma hiyo katika wilaya ya Ilala itafanyika kwa muda wa siku mbili Juni 24 hadi 25, Mwaka huu, ambapo wananchi watapata fursa ya kuonana na madaktari na kufanyiwa vipimo mbalimbali pamoja na kupatiwa matibabu pale itapohitajika.

Zoezi hilo la upimaji wa afya bila malipo katika mkoa wa Dar es salaam, lilianza katika wilaya ya Ubungo, kufuatia wilaya ya Kinondoni na sasa lipo katika wilaya ya Ilala.