Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Kata, kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoendelea kufanya ya kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa pamoja na kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali ya awamu iliyopita.
Pia,Mpogolo amewataka viongozi hao, kutowafumbia macho watu wenye nia hovu na Serikali,hususani baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakisambaza maneno ya kichochezi yenye lengo la kuchonganisha wananchi na Serikali yao.
Mpogolo ameyasema hayo mapema Septemba 18, 2024 Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa semina elekezi kwa Wenyeviti wa Mitaa, Maafisa watendaji na Mabalozi, kutoka Kata tatu za Tabata, Kimanga na Liwiti zilizopo katika Wilaya ya Ilala.
Amesema ni vyema wananchi wakatambua mchango mkubwa unaofanywa na Rais Dkt. Samia katika Taifa na kuwataka kuheshimu Mamlaka zilizo madarakani.
“Rais na Mama yetu Dkt.Samia ni mtu mwenye upendo na ndiyo maana hata alipoingia madarakani alikuta kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu na yeye akaleta yake ya Kazi Iendelee na ndiyo maana tumeona yale yote ikiwemo miradi ya maendeleo iliyoachwa na awamu iliyopita ameiendeleza na mingine imekamilika.
“Ndugu zangu sisi kama viongozi tunawajibu wa kumsemea kwa yale yote mazuri anayofanya, Rais Dkt. Samia ni msikivu na mwenye kujali lakini Kuna baadhi ya watu hawaoni hayo ni kama mtu anayekutoa mkono kwa lengo la kukusalimia alafu wewe unamuwekee moto juu ya huo mkono unategemea nini? Kwahiyo Rais anastahili kulipwa mema kutokana na yale anatoyafanya kwa nchi yake na tusiwafumbie macho wale wanaoletwa chokochoko zenye lengo la uvunjifu wa amani.
Aidha, Mpogolo amewataka viongozi hao kwenda kuhubiri kwa wakazi katika maeneo yao juu ya maadili mema kwa watoto huku akisema kuwa, ukuaji mzuri na utimamu wa akili kwa watoto huanza na wazazi hivyo ni vyema, kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa ajili ya kupata Taifa bora la baadae.
“Niwaombe ndugu zangu viongozi lakini pia na nyie ni wazazi, kwenda kuzungumza na watu wenu katika maeneo yenu juu ya umakini katika malezi ya watoto hususani waliomaliza darasa la saba wanasubiri matokeo kwenda kujiunga na elimu ya Sekondari, kuwe na malezi mazuri ili kuwakinga na mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Tunaposema maadili tunamaanisha kwa mfano, unakuta mama anacheza mziki amenyanyua Dera juu anajifunua maana yake anataka tuone nini?..alafu anacheza hivyo bila kuangalia anacheza mbele ya nani! Watu wazima watafurahia lakini tunawafundisha nini watoto wetu? hili naomba mjifunze na muwe makini nalo ili kukiokoa kizazi chetu”, amesema Mpogolo.
More Stories
RC Mrindoko:Vyombo vya haki jinai shirikianeni kumaliza kesi kwa wakati
RC Katavi ataka huduma ya maji safi na salama iimarishwe kudhibiti Kipindupindu
Walengwa TASAF Korogwe TC watakiwa kuchangamkia fursa