November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KOTTO

DC Mpogolo asisitiza maadili kwa watoto,akemea mimba za utotoni

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Kata, kusimamia maadili ya watoto na kukemea mimba za utotoni.

Mpogolo ameyasema hayo leo Septemba 21, 2024 kwenye mkutano wa viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Kata, uliofanyika eneo la Segerea Jijini Dar es Salaam akimaliza ziara yake aliyofanya katika Kata zote 36 za Wilaya ya Ilala, iliyokuwa na lengo la uelimishaji juu ya uwepo wa mahusiano mazuri kati ya chama na Serikali pamoja na mikutano ya hadhara iliyotoa fursa kwa wananchi kusikilizwa na kutatuliwa kero zao.

Amesema ni vyema kila kiongozi mwenye dhamana akatimiza wajibu wake, ambao ni pamoja na kusimamia maadili ya watoto hususani wa kike ambao kumeonekana kuwa na wimbi kubwa la upatikanaji wa mimba za utotoni na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

” Bado naendelea kusisitiza juu ya kwenda kusimamia maadili mema kwa watoto wetu, watoto wengi wa kike wamekuwa wakikatiza masomo yao kutokana na mimba za utotoni, lakini pia wengi wao takwimu zimeonesha kupatikana na virusi vya UKIMWI na ukichunguza zaidi unakuta watoto wengi wakike wanajihusisha kwenye mahusiano ya kimapenzi na watu waliowazidi umri hii kimaadili si sawa ni vyema tutasimamia maadili”, amesema Mpogolo.

Pia amewataka viongozi hao kutumia nafasi zao kuwaelezea wananchi mafanikio yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo pamoja na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ameipatia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa ajili ya ujenzi wa Shule, vituo vya afya na miundombinu ya barabara.

Amesema, yapo maendeleo mengi yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni vyema juhudi zake zikaungwa mkono.

Aidha, amewataka wananchi kwa ujumla kuwa makini na baadhi ya watu wasiyopenda maendeleo, juu ya kauli za kichochezi zinazoendelea kutolewa, akisema kuwa kauli hizo si nzuri na zina nia ya kuligawa Taifa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

MKUU huyo wa Wilaya leo ikiwa siku ya mwisho wa ziara yake aliyofanya kwa takribani siku nane katika Wilaya hiyo, leo amehitimisha kwa kukutana na Kata ya Segerea, Kinyerezi, Bonyokwa na Kisukuru.