Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ameongoza wananchi wa wilaya ya Ilala
Katika kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika zoezi la kufanya usafi na kupanda miti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na uongozi wa Hospitali, wadau wa usafi .
Akizungumza wakati wa zoezi hilo DC Mpogolo amesema kuwa lengo la kufanya usafi na kupanda miti ni katika kutambua mchango mkubwa unaotolewa Rais Dkt. Samia na Hospitali ya Muhimbili katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi pamoja kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kufanya usafi na kupanda miti katika mazingira yao.
“Tunatambua kazi kubwa ambayo Rais wetu amekuwa akiifanya hasa katika kuboresha sekta ya afya hivyo sisi kama wana Ilala tumeamua kufanya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa kwa kumuombea kwa Mungu ili aendelee kumpa Afya, hekima na maarifa ya kumwezesha kuendelea kuliongoza taifa hili vema,”amesema Mpogolo
Vilevile amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi kwa kuboresha mazingiza ya hospitali na kuhakikisha maeneo yote yanayoizunguka Muhimbili yako katika hali ya usafi.
“Nampongeza sana Prof.Janabi kwa kutambua uhusiano uliyopo baina ya Usafi na Afya, leo tumezunguka maeneo yote ya hospitali ila kila tulipopita hatukuona uchafu wa aina yoyote, hakika Muhimbili ya sasa inapendeza sana,”amesema Mpogolo.
Kwa upande wake Prof. Janabi amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa kushiriki zoezi hilo la usafi na upandaji wa miti na kutoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia swala la usafi ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.
“Kipindi cha Covid 19 magonjwa ya kuharisha na kutapika yalipungua sana kwakuwa watu walikuwa wanafanya usafi na kunawa mikono mara kwa mara hivyo nitumie nafasi hii kuwa kuwasihi kuendeleza utamaduni huo kwakuwa ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu,”amesisitiza Prof. Janabi.
Vilevile Prof. Janabi amewataka wananchi wote wanaokuja Muhimbili kupata huduma ikiwemo wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kuhakikisha kuwa wanatunza mazingira hospitali kwa kuacha tabia ya kutupa taka ovyo na badala yake watupe katika sehemu sahihi.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto