November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo aitaka DAWASA kuimarisha usafi wa Mazingira Buguruni

Na Agnes Alcardo, TimesmajiraOnline,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha usafi wa Mazingira katika eneo la Buguruni Kisiwani.

Mpogolo amesema hayo mapema wiki hii katika ziara yake ya kutembelea na kukagua mradi wa mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka majumbani katika eneo hilo.

“Nawaagiza DAWASA ndani ya wiki hizi mbili kupitia upya mradi huu na kumaliza changamoto zilizobainika na kusababisha mazingira ya Buguruni kuwa katika hali ya kutoridhisha, lakini zaidi niwaombe wananchi kuwa na matumizi sahihi ya miundombinu hii ya majitaka na wao wenyewe kutokuwa sababu ya kufanya izibe mara kwa mara” amesema Mpogolo.

Aidha amesema kuwa, Serikali ilitekeleza mradi wa huo kwa nia njema ya kusaidia wananchi wa maeneo hayo kukabiliana na gharama kubwa za uondoshwaji majitaka zilizowakabili awali, lakini pia kuboresha usafi wa mazingira kwa kumaliza changamoto za utiririshaji majitaka mitaani.

Naye msimamizi wa mradi huo, Charles Makoye, ameeleza kuwa Mamlaka ina mpango wa kufanya maboresho katika mradi huo lakini zaidi kuwa na timu maalumu itakayofuatilia mradi mara kwa mara.

“Pamoja na maboresho tunayoenda kufanya niwaombe wananchi wawe walinzi wa kwanza wa miundombinu hii ili tatizo la uzibaji lisitokee mara kwa mara na majitaka kusambaa mitaani kwani changamoto kubwa ya mradi wetu ni matumizi  yasiyosahihi kutoka kwa wananchi,”mesema Makoye.

Kwa upande wake mkazi wa Buguruni, Aisha Ally, ameishukuru Serikali kwa kufika na kusikiliza changamoto za utitiri wa majitaka mitaani waliyokuwa nayo na kusema kuwa wanaimani na DAWASA watatatua changamoto hiyo kwa wakati kama walivyoagizwa.