
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika futari aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wilayani humo.
Hafla hiyo imefanyika Machi 6, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, na kuwakutanisha waumini wa dini mbalimbali,viongozi wa serikali na makundi mbalimbali ya jamii ili kushiriki sadaka hiyo iliyoandakiwa na kiongozi huyo kwa lengo la kuimarisha mshikamano, umoja na upendo miongoni mwa wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, DC Mbega amewashukuru wananchi wote waliohudhuria tukio hilo, huku akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu katika Wilaya ya Mbozi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Mbozi, Seif Athman, amesema futari ni ibada yenye umuhimu mkubwa katika Uislamu iliyoanza tangu enzi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Ameeleza kuwa ibada hiyo si kwa ajili ya imani pekee, bali pia ni daraja la kuimarisha mshikamano, upendo na umoja kati ya waumini na jamii kwa ujumla.
Aidha, amewakumbusha wananchi kuthamini na kulinda amani iliyopo nchini, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi unaowawezesha wananchi kufanya ibada kwa utulivu, kuishi kwa furaha na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

More Stories
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
Tanzania yaelekezwa kuongeza ushiriki katika biashara ya kaboni kimataifa.
Wanawake wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi