December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc Mbeya: Hakuna mlemavu atakayeachwa kwenye zoezi la Sensa

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imesema kuwa hakuna watu wenye ulemavu ambao wataachwa kwenye zoezi la Sensa la watu na makazi  linalotarajia kufanyika Agosti 23 mwaka huu, na kuongeza kuwa  kila mtu  ajiandae kwa ajili kushiriki na kwamba suala la uratibu kwa kundi hilo linakwenda vizuri.

Imeleezwa kuwa  kundi la watu wenye ulemavu lina wawakilishi kwenye kamati zote zinazohusika na masuala ya uratibu wa maandalizi ya sensa katika wilaya ya mbeya linakwenda vizuri kwa kundi hilo kupitia  wawakilishi  wao .

Akizungumza na majira leo  kuhusiana na maandalizi ya zoezi la Sensa linalotarajia kufanyika  mwezi Agosti Mkuu wa Wilaya ya Mbeya , Dkt.Rashid Chuachua amesema kuwa zoezi hilo litawahusu watu wote wakiwemo watu wenye ulemavu wa aina zote.

‘’Zoezi hili linawahusu watu wote hata kama wanamatatizo  lazima  wahesabiwe, hivyo niiombe jamii itusaidie ili tuweze kuwapata wote, asitokee mtu hata mmoja ambaye atamficha ndani mtu mwenye ulemavu’’amesema Dk. Chuachua.

Aidha Dkt. Chua chua amesema kuwa sensa haiangalii tu idadi ya watu peke yake lakini pia inaagalia rasilimali za watu wanazomiliki, nyumba kwa maana makazi vyoo pamoja na kujua aina ya walemavu kwenye jamii husika, mfano kuna walemavu wasiosikia, viziwi na wengine hivyo ni lazima wote wahesabiwe.
Lilian Mwakitalima, ambaye ni kiziwi amesema hawajapewa mwongozo wa aina yoyote na serikali namna watakavyoshiriki kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi, akieleza taarifa kuhusu mwenendo huo anazipata kupitia vyombo vya habari.

Mwakitalima  akiongozwa na mkalimani wake wa Lugha ya alama amesema  sio viziwi wote wamepata taarifa sahihi kuhusu zoezi hilo angalau wale wenye uelewa kama yeye ndio wanafahamu mchakato huo.

Amesema  kuna umuhimu wa kuwashirikisha viziwi angalau kwa uwakilishi ili iwe rahisi kuwatambua na kuwasiliana na wenzao wakati wa mchakato huo ili kupata taarifa zote muhimu kwa kila kiziwi.
Kwa upande wake , Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ulemavu wa viungo jijini Mbeya, Damas Mwambeje, amesema kupitia umoja wao wameanza kukutana mara kwa mara kwa ajili ya kupeana hamasa ya kushiriki kwenye zoezi la sensa.

Amesema  kwa sasa hakuna takwimu halisi za watu wenye ulemavu, hivyo kupitia sensa serikali itajua idadi yao ili iwe rahisi kuwapa mahitaji yao ya msingi ikiwepo kuratibu swala mikopo ya asilimia mbili zinazotolewa na  halmashauri.

‘’Tumekuwa tukifanya vikao kila baada ya miezi mitatu ili kuhamsishana lakini hata vikao vya kawaida tunapokutana walemavu watatu hadi kumi lazima tusisitize swala la kujiandaa kushiriki zoezi hilo Mwezi wa nane’’ amesema Mwambeje.

Akielezea kwa upande wa Viziwi amesema alikutana nao ili kujua ni kwa namna gani watashiriki kwenye zoezi hilo ambapo walikuja na hoja ya kupata mkalimani kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano wakati wa kuhesabiwa, akiahidi kuwa swala hilo linashughulikiwa na serikali lengo likiwa ni kuondoa vikwazo vyote ili zoezi lifanyike kwa ufanisi.