Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbarali Kanali Maulid Surumbu amesema serikali inatambua changamoto za wazee ikiwepo jamii kushindwa kuwaheshimu,kuwaumiza na kukosa haki zao za msingi baada ya kustaafu.
Kanali ,Surumbu amesema hayo leo,Septemba 27,2024 akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera kwenye Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ruanda Nzovwe Jijini hapa.
Amesema kuwa ni mambo ambayo yanaleta fedhehea ya kiutu huku ikitawaliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba wazee hao wamewalea kwa upendo, uvumilivu ,hali ngumu bila kukata tamaa pamoja na kuwaendeleza mpaka kufikia hatua walizofikia.
Hata hivyo Kanali Surumbu amesema serikali inatambua asilimia kubwa ya wazee wanalea watoto yatima na wasiojiweza pamoja na waliotelekezwa.
Akizungumzia kuhusu mabaraza ya ushauri ya wazee,amesema yamekuwa msaada katika kusuluhisha migogoro na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili hivyo ni wajibu kuhakikisha yanakuwa na vikao kwa mujibu wa mwongozo wa kupokea na kujadili taarifa zake
Aidha Kanali Surumbu amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,Mkoa wa Mbeya una wazee 2,343,754 ambapo kati yao wanawake ni 1,219,926 , wanaume 1,123,828 hivyo idadi ya wazee kuwa asilimia 5.9 ya wakazi wa mkoa Mbeya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la wazee mkoa wa Mbeya ,Arthur Mwankenja amesema bado kuna mambo ambayo yamekuwa yakiathiri ustawi wa huduma kwa wazee ikiwemo watumishi waliostaafu kazi serikalini kutopata mkupuo wa pensheni zao na pia baada ya kupitishwa kikotoo wapo watumishi ambao walitumikia umma kwa zaidi ya miaka 30 lakini huambulia mkupuo wa mil.23 na wengine mil.8 pekee.
Mwankenja pia amesema malipo ya pensheni jamii kwa wazee ambao hawakuwa watumishi wa serikali kama ilivyo Zanzibar wameomba wazee kuanzia miaka 70,ombi hilo lifanyiwe kazi ili kuwaondolea adha wazee hao.
“Tunaomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilifanyie kazi suala hili ili na sisi tuwe kama wenzetu wa Zanzibar wanaopata pensheni tunaamini kupitia baraza hili la wazee tutafikiriwa “amesema.
Ameeleza kwamba mpaka sasa ni halmashauri moja ya Mbarali ndio imefanikiwa kuruhusu wajumbe wawili kutoka baraza la ushauri la wazee kuingia katika vikao vya mabaraza ya madiwani na kwamba baraza hilo linashauri halmashauri zilizobaki kutekeleza takwa hilo la kisera.
Mmoja wa wazee ,Miselina Juma amesema changamoto kubwa walinayo wazee ni matibabu hali inayowafanya baadhi yao kukata tamaa kadi za bidhaa walizonazo zimegeuka kuwa kero kwao kutokana na wanapofika kutibiwa kwenye vituo vya afya na Zahanati huishia kupata vipimo bila kupatiwa dawa.
Maadhimisho ya siku ya wazee Dunini kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Tabora Octoba Mosi mwaka huu huku Kauli mbiu ya siku ya wazee ikisema “Tuimarishe huduma kwa wazee, wazeeke kwa heshima”.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi