Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala,amekabidhi madawati 1525 ambayo yatatumiwa na wanafunzi 4575, katika shule za msingi za wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za uongozi wa Wilaya na wadau mbalimbali katika kuhakikisha watoto wanasoma kwenye mazingira bora.
Madawati hayo ni matokeo ya chakula cha hisani kilichoratibiwa na Mkuu huyo wa Wilaya Mei 31,2022 ambapo madawati,ahadi na fedha taslimu ilikuwa jumla ya madawati zaidi ya 2000.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi madawati hayo iliofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Massala,ameeleza kuwa
wana takwimu ya upungufu wa madawati 5838.
Hivyo wakati wanaendelea na ujenzi wa madarasa waliona waongeze kasi ya sehemu ambayo watoto watakaa ili wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu katika mazingira bora ambayo yamesimamiwa na wazazi wao na viongozi.
Ameeleza kuwa kutokana na takwimu hizo waliona wana wajibu wa kuendelea kuzifuta kama siyo kuziondoa machoni mwao kama viongozi ndio wakaja na mkakati ambao walidhamiria kama mwanzo wapate madawati 1500, hivyo ameshukuru sana tarehe hiyo ambayo waliweza kukutana wakafanikiwa kupata fedha ya madawati ambayo yalivuka lengo.
“Tulikusanya fedha,ahadi,cash pamoja na madawati ambapo jumla ya vyote hivyo ni madawati zaidi ya 2000, mpaka leo tunapozungumza tumefanikiwa kutengeneza madawati 1525 ambayo tumetumia milioni 100, kwa sababu fedha tulichangisha hadharani na madawati tumeona tuyagawe hadharani,”.
“Tumewaita watoto ambao hapo wamekaa watatu watatu na ndivyo inavyopaswa kabla ya hapo watoto hao wakiingia kwenye madarasa wakati mwingine wanakaa wanne au watano kwenye dawati moja na wengine wanakaa chini,”ameeleza Massala.
Pia ameeleza kuwa baada ya madawati hayo watakuwa na uhaba wa madawati zaidi ya 4000 ambapo malengo ambayo wamejiwekea ni kufikia Juni mwakani wawe wamemaliza changamoto hiyo na wanatarajia kuwa na dawati marathon Septemba 10 mwaka huu kwa ajili ya kuchangia madawati.
“Kuna usemi wa kiingereza unasema”If you think, education is expensive try ignorant…. kama unaona elimu ni gharama kubwa sana jaribu ujinga,sisi tumeona tusijaribu ujinga lazima tuwekeze katika elimu,imegawanyika katika maeneo mengi tuna elimu msingi, sekondari mpaka chuo,” ameeleza Massala.
“Ili tujenge Ilemela,ili tujenge Mwanza na taifa ambalo linawatu wenye uelewa na maono lazima tuwekeze kwao na lazima tuanze kuwekeza angali wachanga,leo tumewakusanya hapa ili tushuhudie tulichojaribu kukifanya wote kama watu wa Ilemela,”.
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Buswelu Juliana Anthony,aliahidi kuwa watasoma kwa bidii na kutimiza malengo yote waliojiwekea pia imesaidia kupunguza wanafunzi walioko mitaani kurejea shuleni kwa kuona fursa mbalimbali zinazotolewa shuleni.
“Wanafunzi wenzangu tusome kwa bidii,tuoneshe furaha serikali nawashukuru wote mliotoa michango ya kutuwezesha sisi wanafunzi wa Ilemela tuwe na furaha kwa kutupatia madawati hayo Mungu awabariki,”ameeleza Juliana.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,Fatuma Karoli, ameeleza kuwa Mbunge ameshukuru wadau waliojitoa kuchangia madawati hayo pamoja na Mkuu wa Wilaya huyo mwenye ndoto nyingi na maono kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Ilemela.
“Ni Mkuu wa Wilaya ambaye unajenga na kusimamia utekelezaji wake,leo tunashuhudia utekelezaji wa madawati hapa Ilemela, Mbunge yupo na wewe bega kwa bega katika kila ndoto ambayo utafikiria kuisaidia Ilemela,”ameeleza Fatuma.
Kwa upande wake mmoja wa wadau waliochangia madawati hayo Meneja wa Benki ya Stanbic tawi la Mwanza Geofrey Makondo,ameeleza kuwa amepongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa maono na usimamizi wake ambao amefanikisha watoto kupata madawati.
“Nakushukuru kwa sababu unayoyafanya ni kwa ajili ya taifa naamini watoto hawa kwa kupata madawati watasoma vizuri na uelewa utaimarika,kwenye takwimu bado tunaupungufu wa madawati,vyumba vya madarasa na nyumba za walimu, wadau wenzangu niombe tuendelee kujitoa tusichoke,”ameeleza Makondo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa