December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Masalla: Tunaendelea kukabiliana na makundi ya uhalifu

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla,ameeleza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo inaendelea kukabiliana na makundi mbalimbali ya uhalifu ili kuhakikisha wananchi wanabaki salama.

Huku akikemea vitendo hivyo vya uhalifu vinavyofanyiwa na makundi hayo sanjari na kutoa wito kwa wazazi kuhakikisha inawalewa watoto wao katika maadili ili kuwaepusha kujiingiza katika ufanyaji wa vitendo vya uhalifu.

Masalla ametoa kauli hiyo mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kata ya Nyasaka juu ya uwepo wa makundi ya vijana yanayojihusisha na vitendo vya uhalifu,wakati wa mkutano na wananchi hao ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea Kata na Mitaa ndani ya Wilaya hiyo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu.

Amesema,wakiwa ndani ya Nyasaka wamepokea changamoto inayohusiana na makundi ambayo yanajihusisha na uhalifu ambayo wameyasikia kuwa kuna kundi linajiita G7, sanitizer,barakoa na majina kama ya namna hiyo kwenye miji mikubwa kama Dar-es-Salaam inajulikana kama panya road.

“Kimsingi hayo ni makundi ya kihalifu na bahati mbaya sana wanaojishughulisha na makundi haya ni watoto wadogo, hii yote ni kwa sababu ya changamoto ya matumizi ya madawa ya kulevya na bangi”amesema Masalla na kuongeza kuwa

“Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya tumejipanga kuendelea kukabiliana na makundi ya namna hiyo na kuhakikisha watu wanabaki salama,ambapo zaidi ya vijana 30 tayari tumeisha wakamata lakini bado tunaendelea kuwatafuta vijana ambao bado kimsingi wapo katika mitaa yetu,”.

Pia amesema,vijana au watoto hao wanatoka miongoni mwa jamii na wanawafahamu hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili waendelea kufanya uchunguzi wa chini kwa chini na wawachukulie hatua vijana wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Wazazi ni jukumu letu kulea watoto kwenye maadili pia viongozi wa dini na jamii kwa ujumla,siyo suala la kumuachia mtu mmoja mpaka mtoto anafikia hatua ya kushika panga na kuingia mtaani na kwenda kufanya uhalifu maana yake ni kwamba jamii inayomzunguka jambo hili inakuwa imesha liona lakini wanashindwa kukemea na kuchukua hatua,”amesema Masalla.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilemela SSP. Elisante Ulomi, amesema, wanaendelea na oparesheni kubwa ya kumatata vijana wanaojihusisha na uhalifu ambapo wamewakamata vijana zaidi ya 50 wenye umri kati ya miaka 17 hadi 23 ambao wameunda makundi hayo ya kihalifu yakiwemo G7, Selebobo, Sanitizer,Barakoa na Covid.

Amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwaendekeza watoto wao huku akihoji kuwa unanunuliwaje simu na mtoto wakati unajua mwanao hafanyi kazi mwanao yupo shuleni hao barakoa na Covid wameanza kwenye shule,sasa inakuwaje mwanafunzi anakuwa sehemu ya kutengeneza kundi la uhalifu huku akisisitiza kuwa jambazi ata awe sugu vipi lakini anamsikiliza mama yake hivyo ametoa wito kwa mama kutumia nafasi yake kumueleza mtoto aache uhalifu.

“Watu wanaofanyiwa vitendo hivyo wanafika mahali wanachoka haturuhusu vitendo vya kujichukulia sheria mkononi,lakini mzazi usilaumu mtu, usilaumu serikali,jeshi la polisi na wananchi wenzako mpaka mtoto anafikia hatua ya kufanya uhalifu maana yake kuna sehemu moja au nyingine ujatimiza wajibu wako ujamkanya anafanya vitendo vya uhalifu anakuja na mali nyumbani umuulizi hivi vitu vimetoka wapi unampokea,anakuhudumia kwa vitu hivyo vya uhalifu mwisho wake anakuja kufika mahali anapigwa aturuhusu kabisa kupiga wezi mlete mkondo wa sheria utaamua,” amesema Ulomi.

Aidha amesema, viongozi wa dini,wananchi, viongozi wa serikali za mitaa kila mmoja kwa nafasi yake washirikiane kuwafichua na kutoa taarifa za wanaofanya uhalifu pia wanaonunua simu na vitu vya wahalifu kwani vitendo hivi pia vinasababishwa na matumizi ya dawa za kulevya na bangi.

“Niombe tuendelee kupata taarifa za wanaojihusisha na matumizi, usafirishaji na uuzaji wa bangi hao wote tushughulike nao,nawaombeni sana ushirikiano tukiweza kukomeshe hivi vitendo tutakuwa na Nyasaka ambayo haina uhalifu,”amesema Ulomi.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla, akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyasaka katika mkutano na wananchi hao ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea Kata na Mitaa ndani ya Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu uliofanyika Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza. (Picha na Judith Ferdinand.)
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilemela Elisante Ulomi,akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyasaka juu ya uwepo wa makundi ya vijana yanayojihusisha na uhalifu katika mkutano na wananchi hao na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea Kata na Mitaa ndani ya Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu uliofanyika Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza. (Picha na Judith Ferdinand.)
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyasaka waliohudhuria mkutano kati ya wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea Kata na Mitaa ndani ya Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu uliofanyika Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand.)