December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ludigija: Maeneo yenye mikusanyiko wekeni vifaa vya kidhibiti moto

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzi Ludigija ameyataka maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu ambayo yamekuwa yakitoa huduma kuwekwa vifaa vya kuzidhibiti moto ili kujiepusha na majanga yanapotokea.

Ludigija ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam leo Mei 19 wakati wa kilele Cha maadhimisho ya siku ya Zimamoto Mkoa wa Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na kutoa elimu kwa Wananchi namna ya kukabiliana na majanga ya moto.

Amesema maeneo ambayo yanapaswa kuwekwa vifaa hivyo kuwa ni hospitalini, vituo vya afya, standi, Sokoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko.

“Nalielekeza Jeshi la Zimamoto na uokoaji kuchukuwa hatua kwa Taasisi au Wananchi wanaokaidi maelekezo ya Jeshi Hilo hususani kuweka Vifaa vya kudhibiti moto kwenye maeneo ya Biashara na Majengo marefu”amesema

Aidha alizitaka Halmashauri jijini Dar es Salaam kusimamia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), ili zishirikiane kujenga visima vya maji kwa ajili ya mahitaji ya zimamoto pale janga linapotokea”alisema

Hata hivyo Ludigija alilitaka zimamoto kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaokaidi maelekezo yanayotolewa na jeshi hilo hususan kwenye maeneo ya biashara.

“Kuna baadhi ya watu wanakaidi maagizo ya kisheria yanayotolewa na zimamoto hivyo likitokea janga hasara ni kubwa,” amesema

Amesema mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni ya mikoa inayotegemewa nan chi kiuchumi.Katika hatua nyingine Ludigija aliwataka Wananchi kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa mapema pindi wanapobaini tukio la moto ili kuwezesha Zimamoto kufika kwa wakatina kuokoa Maisha ya Wananchi na Mali.

Naye Mkuu wa Chuo cha Zimamoto, Kenedy Komba amesema katika maadhimisho hayo wameweza kutoa kadi ya bima kwa watoto 30 waliolazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kutokana na ajali za moto pamoja na watoto wengine waliolazwa hospitalini hapo kwa kutoa vifaa mbalimbali vya tiba.

Akitaja baadhi ya vifaa tiba hivyo ni pamoja na nepi, kanga pamoja na sabuni .

Awali Kamishina msaidizi Mwandamizi kamanda Elia Kakwembe kutoka zimamoto na uokoaji viwanja vya ndege amesema katika maadhimisho hayo wamekuwa wakitoa elimu na kuhabarisha umma namna Huduma za zimamoto na uokoaji zinavofanyika katika viwanja ndege.