November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kinondoni awapongeza wakazi Bunju B

Na Joseph Kayinga,TimesMajira Online, Dar

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe amepongeza juhudi za wakazi wa Mtaa wa Bunju B kufanikisha ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa kwa kujitolea nguvukazi, vifaa vya ujenzi, pamoja milki ya ardhi.

Pongezi hizo zilitolewa wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ikiongozwa na yenye mwenyewe kwa lengo la kukagua shughuli za maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Wakielezea walivyofanikisha mradi huo wa ujenzi unaokadiriwa kugharimu mamilioni ya shilingi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bunju B Bw. Athuman Juma Njama alieleza kuwa mpaka siku ya ukaguzi huo gharama zote zilichangiwa na wananchi na taasisi zilizopo mtaani hapo.

Akifafanua maelezo hayo Njama alibainisha kuwa Kiwanja ilipojengwa Ofisi hiyo ya Mtaa kilitolewa Bure na familia ya Bw. na Bi Mwakalinga ambao ni wamiliki wa shule ya Msingi ya TEJ.

Vifaa vya ujenzi ikiwemo Saruji, matofali, mbao, misumari, bati na gharama za ufundi zimebebwa na wananchi pamoja na wamiliki wa kituo Cha mafuta cha Meru petrol station Mzee Kaboko na wenzake pamoja na Kampuni ya Times Valley.

Akielezea kufurahishwa na juhudi hizo Gondwe alielekeza watendaji wa Manispaa Kinondoni chini ya Mkurugenzi wafike mtaani hapo kukamilisha urasimishwaji wa Ofisi hiyo kisheria.

Pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa viongozi wengine waliokuwepo ni Mtendaji wa Mtaa Raphael Mchomvu, mjumbe Juma Songo pamoja na Halima Mnikita.

Kwa upande wa wananchi na wadau Mama Mwakalinga ameeleza kuwa wao kama wamiliki wa shule ya Msingi ya TEJ walipenda kuona Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Bunju B inakuwa na sura inayolingana na Hadhi ya kisasa.