December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kilindi ataka nguvu iongezwe ukusanyaji mapato

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Kilindi

MKUU wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Hashim Mgandilwa amesema pamoja na Halmashauri ya Wilaya hiyo kukusanya mapato kwa asilimia 131 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, bado wanatakiwa waongeze nguvu ya ukusanyaji wa mapato hayo.

Lakini pia, wilaya hiyo ina miradi mingi ambayo haijakamilika, hivyo badala ya kushughulika na miradi mipya, basi waangalie namna ya kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya zamani, kwani miradi hiyo inahitaji fedha kidogo ili kuikamilisha.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha Baraza la Madiwani robo ya nne, na kuongeza kuwa timu za ukusanyaji mapato ziongezewe nguvu, kwani bado kuna mianya kwenye ukusanyaji mapato, hasa minada ya mifugo.

Amesema, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilipanga kukusanya sh. 2,725,024,000 kama mapato ya ndani, lakini imeweza kukusanya sh. 3,565,400,292 sawa na asilimia 131, lakini bado haitoshi, kwani wilaya hiyo ni kubwa na ina vyanzo vingi vya mapato.

“Leo tunajisifu kwa kusema tumeweza kukusanya mapato makubwa sana, tunazungumzia habari ya asilimia, tunasema tuna mapato mengi sababu tumekusanya asilimia 131, lakini tukiulizwa kile tulichokikusanya ni shilingi ngapi, ni karibu sh. bilioni 3.5. Ukiangalia bil. 3.5 kwa ukubwa wa wilaya hii fedha hiyo ni ndogo, na tunaweza kukusanya mapato makubwa, ili mradi sote fikra yetu iwe kwenye kukusanya mapato.

“Kwa hiyo madiwani niwaombe mlichukulie hili kwa uzito, msaidie hizi timu za ukusanyaji mapato ziweze kufanya kazi vizuri katika ukusanyaji mapato. Pamoja na hilo, lakini bado hatujafanya vizuri sana hasa kwenye ushuru wa mifugo. Ukienda minadani bado kuna mianya mingi sana katika ukusanyaji mapato. Niombe Mwenyekiti (wa Halmashauri ya Kilindi Idrissa Mgaza), wakati tunaanza mwaka mwingine (2024/2025) tuweke mikakati mizuri ili mwisho wa siku tuweke usimamizi mzuri wa ukusanyaji mapato” amesema Mgandilwa.

Mgandilwa amesema wilaya hiyo ina miradi mingi ambayo haijakamilika, hivyo badala ya kushughulika na miradi mipya, basi waangalie namna ya kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya zamani ili iweze kukamilika, kwani miradi hiyo inahitaji fedha kidogo ili kuikamilisha na wananchi kupatiwa huduma.

Akijibu baadhi ya maswali ya madiwani ya papo kwa hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi John Mgalula amesema wanatafuta fedha ili kukamilisha majengo matatu Kituo cha Afya Kwediboma, jengo la maabara na jengo la upasuaji.

Mgalula pia amemuahidi Diwani wa Kata ya Kwediboma, Mwajuma Sempule, kuwa gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kwediboma watalitengeneza baada ya mifumo kufunguka, kwani gharama ya matengenezo ni zaidi ya sh. milioni tisa.

Kwenye swali lake, Sempule aliuliza, pamoja na Serikali kujenga Kituo cha Afya Kwediboma, bado kuna majengo hayajakamilika likiwemo la maabara, upasuaji, na Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) ambalo lilijengwa kwa nguvu za wananchi. Lakini pia waliahidiwa kupewa gari la wagonjwa kwenye kituo hicho.